Mkutano wa viongozi wa Afrika umeanza mjini kuangazia mzozo unaokumba Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hizi ndizo juhudi za hivi karibuni kujaribu kumaliza mgogoro ambao umekumba eneo hilo kwa miaka mingi.Rais wa DRC, Joseph Kabila na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame wanahudhuria mkutano huo wakati Kinshasa ikishutumu Rwanda kwa kusaidia wanajeshi waasi kuchochea vurugu .
Mkutano huu ambao Rais Yoweri Museveni ndiye mwenyeji, utazingatia mapendedezo yaliyotolewa kwenye mikutano ya awali ambayo haijaweza kupiga hatua katika kuunda kikosi cha kimataifa cha kujitegemea kuweza kukabiliana na hali.
Eneo la Mashariki mwa Congo, limekumbwa na uasi mkubwa unaoendeshwa na wanajeshi walioasi jeshi na ambao wameunda kundi la M23,ambalo wanachama wake ni wapiganaji wa zamani wa kitutsi, walioingizwa katika jeshi la serikali chini ya mkataba wa amani ulioafikiwa mwaka 2009.
Bosco Ntaganda, anayesakwa na mahakama ya kimataifa ya ICC, kuhusu mashtaka ya uhalifu wa kivita, anatuhumiwa kwa kuongoza kundi la M23.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Juni, ilituhumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi, na kuchochea mgogoro katika nchi jirani ya DRC.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na mwenzake wa Sudan Kusini Salva Kiir pia wanahudhuria mkutano huo pamoja na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete .
Mkutano huu ni wa nne katika kipindi cha miezi mitatu ulioandaliwa na kongamano la nchi kumi na moja kuhusu Maziwa Makuu na unakuja baada ya mkutano ulioandaliwa mwezi jana kwa ushirikiano na baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment