Saturday, December 15, 2012

Waziri matatani-ni Lazaro Nyalandu kwa kumiliki kampuni ya utalii


NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (pichani) anadaiwa kumiliki kampuni inayojishughulisha na masuala ya utalii kitendo ambacho kinamwingiza kwenye mgongano wa kimasilahi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Nyalandu anamiliki Kampuni ya Nitoke Safaris Ltd jambo ambalo limeelezwa kuwa ni kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma hasa kwa kuwa yeye ni msimamizi wa sekta hiyo.
Taarifa kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni na Leseni (Brela), zinaonyesha kuwa wamiliki wa Kampuni hiyo ni L.S.Nyalandu na Faraja G. Nyalandu, huku kila mmoja akimiliki asilimia 30 ya hisa.
Kampuni hiyo ilisajiliwa Aprili 24, 2009 na kupewa nambari 70735, wakati huo Nyalandu akiwa Mbunge wa Singida Kaskazini, wadhifa alioupata kuanzia mwaka 2000.
Ofisi za kampuni hiyo ziko PPF Complex Suit, namba 24 Barabara ya Mzingo, Arusha na magari ya kampuni hiyo yamekuwa yakibeba watalii mkoani Arusha.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo jana akiwa Mwanza, Waziri Nyalandu alikiri kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo lakini akasema tayari alishajitoa.
Katika kujenga hoja ya utetezi wake, Nyalandu alisema kama ambavyo haipendezi yeye kumiliki kampuni ya utalii akiwa waziri wa wizara hiyo, haitapendeza pia waziri wa habari kumiliki gazeti.
“Huwezi kuwa Waziri wa Utalii na ukafanya biashara ya utalii huko katika kampuni hiyo mie nilishatoka kitambo,” alisema bila kufafanua zaidi.
Hata hivyo, kumbukumbu za Brela zinaonyesha kuwa waziri huyo bado ni mmoja wa wanahisa ingawa haijafahamika kama ni tatizo la Brela kutorekebisha kumbukumbu za jalada lake baada ya kujitoa au la.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki alipoulizwa na gazeti hili jana alionyesha kushtushwa na taarifa hizo na kusema hajui kama Naibu wake anamiliki kampuni ya utalii.
“Siwezi ku comment (kutoa maoni), chochote juu ya jambo hilo kwa sababu sijui kama ana kampuni ya utalii na pili, ndiyo kwanza nasikia hizo taarifa kutoka kwako (mwandishi),” alisema Kagasheki.
Taarifa zilizowakariri baadhi ya mawakala wa utalii mikoa ya Kilimanjaro na Arusha zilidai kuwa Nyalandu ni mmoja wa washindani katika biashara hasa ya kwenda mbuga za wanyama
Haijafahamika kama Nyalandu aliwahi kutangaza kuwa na masilahi na kampuni hiyo au kama aliwahi kuiorodhesha kama moja ya mali anazomiliki kama Sheria ya Maadili ya Viongozi inavyotaka.
“Siyo tatizo kiongozi kumiliki kampuni, lakini unatakiwa ku-declare interest (kutangaza masilahi) lakini kwa Nyalandu ni tofauti kidogo kwa sababu sasa yuko kwenye sekta hiyo,” alidokeza wakili mmoja.
Wakili huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema hata kama Nyalandu atakuwa haipi upendeleo kampuni hiyo, lakini kwa akili ya kawaida, ni rahisi binadamu kuhisi kampuni hiyo itakuwa ikipewa upendeleo wa aina fulani.

No comments:

Post a Comment