PADRI Ambrose Mkenda ambaye alipigwa risasi Jumanne iliyopita,
mjini Zanzibar na watu wasiojulikana amekana maelezo yaliyotolewa na
polisi yakimtaja kuwa ni Mhasibu wa Kanisa Katoliki, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako amelazwa, Padri huyo alisema wadhifa wake ni Mkurugenzi wa Idara ya Uchungaji anayeshughulikia masuala yote ya Kanisa Katoliki visiwani humo.
Alisema hakuwa mhasibu wa kanisa hilo kama inavyoelezwa na kwamba taarifa hizo siyo za kweli.Hata hivyo, Padri Mkenda alisema alikuwa akimsaidia mhasibu kwa kipindi cha miezi mitatu.
“Mimi sikuwa mhasibu wa kanisa kama inavyoelezwa na watu. Napinga vikali taarifa hizo kwani mimi nilikuwa namsaidia mhasibu kwa muda tu kwani hakuwapo,” alisema.
Alipoulizwa jana kuhusu madai hayo mapya ya Padri Mkenda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohamed alisema asingeweza kuzungumza lolote kwa kuwa alikuwa nje ya kituo chake cha kazi licha ya kuwa na jibu la madai hayo.
“Sasa nipo Dar es Salaam kikazi. Naogopa kuandikwa kwamba nimetoa ufafanuzi juu ya suala uliloniuliza. Japokuwa majibu ninayo, lakini cha msingi ni kwamba jaribu kumtafuta kaimu wangu Haji Hana anaweza kuwapa majibu,” alisema Mohamed.
Alipoulizwa Kamanda Hana alisema inawezekana madai ya Padri Mkenda yakawa ya kweli kwa kuwa baada ya tukio hilo hakuweza kuzungumza lolote na badala yake maelezo yake yalitolewa na wasaidizi wake ambao ndiyo waliosema kwamba alikuwa mhasibu.
“Padri alikuwa akizungumza kwa ishara, hivyo hakuweza kusema chochote. Wasaidizi wake ndiyo wakatoa taarifa hizo kwamba ni mhasibu wa Kanisa.”
Akizungumzia hali yake Padri Mkenda alisema anaendelea vizuri lakini bado ana maumivu makali katika sehemu za mwili wake ikiwa ni pamoja na kichwani.
SMZ yatoa tamko
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema inafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwa Padri Mkenda.
Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kumjulia hali Padri Mkenda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud alisema Serikali inafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
Alisema kwa sasa ni mapema kujua chanzo cha tukio hilo kwani tayari vyombo vinavyohusika ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi Zanzibar na Tanzania Bara vimeshapewa jukumu la kufanya uchunguzi.
“Tukio hili ni kubwa na limetuhuzunisha. Kwa kutambua umuhimu wa watumishi wa dini nchini, Serikali inafanya uchunguzi wa kina ili kutambua chanzo cha tukio hilo haraka,” alisema Aboud na kuongeza:
“Kwa sasa ni vyema tukawaachia madaktari ili wandelee na uchunguzi wa afya yake lakini ifahamike wazi kwamba Serikali ipo makini na pindi wahusika watakapopatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria.”
No comments:
Post a Comment