Friday, December 28, 2012

Lema amsikitikia anayedaiwa kuwa askari JWTZ Monduli

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amesema kama angekuwa ndiye mwenye uamuzi ya mwisho ndani ya Chadema, angempokea kwenye chama hicho askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), aliyepiga naye picha kama kitendo hicho kitamfanya afukuzwe kazi.
 
“Ingawa wanaofaa kutoa kauli kama hizi ni viongozi wakuu kama Mwenyekiti na Katibu wa Taifa kupitia vikao halali vya chama, lakini binafsi, ningekuwa na uwezo, ningempokea mara moja askari huyu kwenye chama kama ishara ya walio tayari kujitoa mhanga kupoteza vyote ikiwemo kazi kwa ajili ya ukombozi wa taifa iwapo atafukuzwa kazi,” alisema Lema.
Hata hivyo, Lema aliyekuwa akizungumza katika mahojiano maalumu akiwa mjini Moshi kwa mapumziko ya Sikukuu ya Krismasi, alisema kitendo cha JWTZ kuanza kumwandama na pengine kumfukuza kazi askari huyo, kitafumua chuki kubwa kati ya askari wa vyeo vya chini na wenye vyeo vya juu ambao wengi wanaitumikia CCM kwa nafasi zao, ukiwemo ukuu wa mikoa na wilaya.
Alitoa mfano Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Samuel Ndomba ambaye kabla ya kuhamishiwa Makao Makuu ya jeshi alikoshika nyadhifa mbalimbali na hatimaye kuteuliwa kushika nafasi yake ya sasa, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, cheo kilichompa fursa ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati ya siasa mkoa wa CCM, Mkoa wa Arusha.
“Askari huyu mdogo akifukuzwa kazi kwa sababu ya picha aliyopiga na sisi, basi itathibitisha double standard (undumila kuwili)  ya utawala katika taifa letu. Huyu kapiga picha na taarifa ya kusakwa inatolewa na JWTZ , lakini wako wengi ambao ni wanajeshi wa vyeo vya juu ambao siyo tu wanapiga picha na viongozi wa chama tawala bali ni wafanyakazi wa CCM kwa nyadhifa zao wakiwa bado wako jeshini,” alisema Lema.
Alisema ujasiri wa mtu huyo anayeamini kuwa kweli ni askari wa JWTZ kujitokeza kupiga naye picha huku akijua anahatarisha kazi yake, ni ushahidi kuwa wapo askari wengi nchini  waliochoshwa na mwenendo wa CCM.
Alisema ukweli huo unathibitishwa na matokeo ya kura katika vituo vilivyokuwa ndani au jirani na vituo vya polisi na kambi za jeshi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, ambapo wagombea wa upinzani walipata kura nyingi ikilinganishwa na wale wa CCM.
Lema aliyepiga picha na askari huyo akiwa na mbunge mwenzake wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), alitoa changamoto kwa watu wenye mapenzi mema na taifa hili, kufanya utafiti wa maofisa wa juu wa JWTZ na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanaotumikia chama tawala kwa siri au kwa uwazi kupitia vyeo na nyadhifa zao.
“Hawa ni pamoja na wakuu wa mikoa, wilaya na maofisa wa ngazi mbalimbali ndani ya CCM ambao tunashuhudia wakirejea jeshini wakitokea kwenye utumishi wa chama lakini hatujawahi kusikia tamko la kutafutwa wala kuchunguzwa na jeshi kwa kushiriki siasa,” alisema Lema
Alisema hata ikitokea kweli askari aliyepiga naye picha akafukuzwa kazi hatajuta kumsababishia madhila hayo bali atajisikia faraja kwa sababu kitendo hicho kitafungua ukurasa mpyae katika harakati za ukombozi kwa watu kuelewa kuwa siyo kila jaribu au makosa ni mkosi, bali ni hatua muhimu katika kufikia mafanikio ya unachokiamini.
Alisema askari huyo atakuwa ameshinda hofu, vitisho na uoga alivyosema ni miongoni mwa dhambi kuu katika maisha ya mwanadamu na kuwataka Watanzania kutoogopa lolote, hata ikibidi kifo wakati wakipigania haki zao kwani hakuna atakayeishi milele kwa kuogopa kufa.
“Ni heri mtu kuishi miaka michache duniani na Jina lake kubaki linaishi kwa haki na wema kuliko kuishi miaka mingi akatoweka kama mzoga” alisema Lema akimkariri Mwana mapinduzi Steve Biko na kuongeza  “Ni dhambi kubwa katika demokrasia kuupuuza ukweli eti kwa sababu anayesema uongo amejifunza kupiga na kuua,”
Lema aliishauri JWTZ kutekeleza ahadi ya kulinda Taifa hata kwa kukemea kwa maneno wizi wa mali na rasilimali za umma zikiwemo fedha na wanyapori wanaotoroshwa kwenda nje kwa msaada wa waliokabidhiwa dhamana ya kuvilinda na kuvitunza kwa faida ya wote.

No comments:

Post a Comment