Monday, December 10, 2012

Kata nane ziko wazi nafasi ya udiwani – Nec


Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza nafasi nane za udiwani kwamba ziko wazi; tano zikiwa ni za kata, ambazo zinatakiwa kujazwa kupitia uchaguzi mdogo na tatu za viti maalum, zinazotakiwa kujazwa kupitia uteuzi wa chama husika.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Oigenia Mpanduji, kata hizo zimekuwa wazi kutokana na madiwani waliokuwa wakiziwakilisha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufariki dunia.

Pia kati ya nafasi tatu za viti maalum, mbili zilizokuwa zikiwakilishwa na madiwani kupitia CCM zimekuwa wazi baada ya mmoja wao kupoteza sifa na mwingine kufariki dunia.

Vilevile, nafasi moja ya viti maalum iliyokuwa ikiwakilishwa na diwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imekuwa wazi baada ya diwani wake kuvuliwa uanachama.

Mpanduji alisema hayo alipozungumza na NIPASHE ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana na kusema taarifa ya nafasi hizo kuwa wazi zimepokelewa na NEC kutoka ofisi ya waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa.

Alizitaja kata, ambazo ziko wazi zinazotakiwa kufanyiwa uchaguzi kuwa ni Langiro iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma; na Manchila iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

Nyingine ni Iyela iliyoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Mbeya, mkoani Mbeya; Mbalamaziwa iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa na Runzewe Mashariki iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.

Nafasi za diwani viti maalum zilizo wazi, ambazo zinatwakiwa kujazwa alizitaja kuwa ni pamoja na iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera (CCM); Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (CCM) na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (Chadema).

Hata hivyo, Mpanduji alisema NEC bado haijakutana ili kupanga tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi kujaza nafsi hizo.

Kwa mujibu wa Mpanduji, uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hizo, unaweza kufanyika mwakani.
Alisema hali hiyo inatokana na sheria kuruhusu uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani kufanyika mara mbili kwa mwaka, ambazo kwa mwaka huu, ulifanyika Aprili Mosi na Oktoba 28.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment