Nitalizungumzia katika sura mbili; kwanza
pale mtu anapodai mtoto huyu siyo wangu kwa maana hafanani naye na pale
mwingine anapohoji mlo huu umetoka wapi pale anapokuwa hajatoa fedha ya
matumizi.
Mambo hayo mawili yamekuwa yakizitesa sana
familia nyingi na hata kusababisha kusambaratika kwa familia ama
kutengana au hata ndoa kuvunjika kabisa.
Naam. Lipo suala la mtoto anazaliwa, kisha
baba watoto anakataa eti siyo wa kwake kwa sababu hana sura yake. Hivi
majuzi nilisikia jamaa wakibishana juu ya kisa cha mwenzao aliyemfukuza
mkewe eti kamzalia mtoto mweupe badala ya mweusi tofauti na watoto
wengine.
Jamaa huyo ikaelezwa kuwa alioa ndoa ya
nguvu miaka saba iliyopita na wakabahatika kupata watoto wawili ndani ya
miaka mitano. Mwaka mmoja uliopita wakabahatika tena kupata mtoto wa
tatu. Lakini mtoto huyu kadiri anavyokuwa, anazidi kuwa mweupe wakati
wenzake wana weusi wa baba na mama yao. Tena eti pua ni ndefu tofauti na
wengine.
Baba kuona hivyo ndipo akaanza kuhoji;
“Mbona mtoto anazidi kuwa mweupe wakati sura za wenzake ni weusi? Na
hiki kipua nacho vipi?
Mkewe alijitahidi kujitetea, tena
aking’ang’ania kuwa anafanana na babu anayemzaa mamake, lakini mume
hakukubali na hivyo majuzi kumtimulia kwao hadi jambo hilo lijadiliwe
kifamilia. Ndipo jamaa hawa wakawa wanamrushia madongo jamaa kwa hatua
hiyo ya kikatili.
Nilipoondoka mahali pale nikawaza: Jamaa
analalamika kuwa mtoto hana sura yake, je, yeye alikuwa wapi hadi mtoto
azaliwe na sura isiyo yake ndani mwake? Hivi jamaa alikuwa anawajibika
ipasavyo kindoa au alikuwa kiruka njia na anapotua nyumbani anakuwa
‘chaka mbaya’? Kama ndivyo, kwanini alalamike wakati ndoa anaibomoa
mwenyewe?
Katika mazungumzo ya wale jamaa, mmoja
nilimsikia akisema; “Sisi tunamjui ni mchapaji sana huko nje na siyo
ajabu akirudi nyumbani kachoka na hatoi huduma stahiki kwa mkewe. Sasa
mama huyu atamsubiri asiyemuona hadi lini? Huduma hafifu ndizo kichocheo
cha mama kuchepuka nje anapopata uchochoro”. Ama kwa hakika Maisha
Ndivyo Yalivyo. Au siyo msomaji wangu?
Suala lingine linalotesa familia zetu, ni
ile tabia ya baadhi ya kinababa kuhoji “msosi huu umetoka wapi” wakati
hata ndururu(senti) hajaacha kwa ajili ya matumizi.
Tena tabia hii imejiimarisha sana kwa wale
ama kipato chao ni cha kubangaiza, au wataafu ambao hawakujiandaa
kustaafu na hata pale walipostaafu na kupata mafao yao, wakayatapanya
pasipo mpangilio wa kuwekeza ili wajiendeleze kiuchumi. Matokeo yake
wanawavuruga hata wake zao ambao wanajitahidi ili maisha yasonge mbele.
Hakuna asiyetambua jitihada za kinamama
katika kujiendeleza kiuchumi. Wengi wamejikita katika miradi mbalimbali
ya kijasiriamali na hivyo kuwa nguzo muhimu katika pato la familia.
Wapo baadhi ya kinababa ambao wakitoka, wametoka hadi usiku. Haachi hata seti lakini akirudi nyumbani lazima anadai chakula.
Ni vema basi unaporudi na kukuta
vimeandaliwa mezani usihoji kwa makeke eti vimetoka wapi? Tena anakuwa
mkali wakati hakuacha hela ya matumizi pengine yapata wiki sasa. Je, hii
ni haki? Tena haulizi kwa polepole aeleweshwe, anabwatuka nusura
ambutue mtu…Ebo!
Katika familia zingine, utakuta baba anao
uwezo wa kuacha hela ya matumizi lakini kutokana na kuwa na nyumba ndogo
anayoithamini zaidi, huegemea huko na kutojali pale anapoamkia nyumbani
kwake. Sasa kwanini mama hata ikiwezekana asikope gengeni au buchani
ili mkono uende kinywani?
Na hali hii ya maisha ndiyo inayopelekea
kuzaliwa watoto wasiofanana na baba mwenye nyumba. Kumbe mama afanyeje
wakati msosi unahitajika nyumbani, baba katimka hakuacha hela ya mboga,
akirejea na kukuta mchuzi wa nyama na vikolombwezo vingine atahoji kwa
makeke yapi? Tuache utani!
Mpenzi msomaji, maeneo hayo mawili
nimeyaunganisha tuyajadili kwa sababu yanachangamana. Baba haonekani
nyumbani, akizaliwa mtoto wa sura tofauti anapiga kelele. Baba haachi
hela ya mboga, akirejea na kukuta msosi wa kuku anapiga kelele. Yeye
alikuwa wapi hadi anapatiwa ufadhili? Hebu msomaji wangu toa maoni yake
kuhusu maeneo hayo tuelimishane.
Ukiwa tayari kwa maoni, kuwa
huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi
namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
Wasalaam.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment