Monday, December 10, 2012

Zitto awalipua Wazungu

  *Ni uporaji wa matrilioni
                                                                          Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe
Waziri  Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe, amewalipua Wazungu kuwa ni waporaji wakubwa wa rasilimali za Afrika.

Pia ameitaja Uswisi moja kwa moja kwa moja kuwa inakumbatia sera ambazo zinasaidia uporaji wa rasilimali hizo kwa kuweka vivutio vya kutokulipa kodi na taratibu ngumu na zisizo wazi katika kufuatilia fedha zilizoporwa katika mataifa ya Afrika.

Alisema uporaji huo kwa kiasi kikubwa unaziumiza zaidi nchi nyingi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa njia ya ukwepaji kodi, rushwa na hila nyingine katika sekta ya uwekezaji.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa masuala ya ushirikiano wa uchumi kati ya Ujerumani na nchi za Afrika.

Mkutano huo wa siku tatu mfululizo, kuanzia Desemba 9, mwaka huu, unafanyika mjini Berlin, nchini Ujerumani.

Zitto anatoa kauli hiyo wakati kukiwa na harakati kubwa nchini za kutaka Watanzania walioficha zaidi ya Dola bilioni 300 katika mabenki ya Uswisi wawajibishwe ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa fedha hizo nchini.

Miongoni mwa watu wanaodaiwa kuficha fedha hizo Uswisi ni pamoja na watumishi wa umma na viongozi waandamizi.

Katika mkutano wa jana, Zitto alisema kuwa nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikiporwa maliasili zake na baadhi ya kampuni za kimataifa kupitia ukwepaji kodi pindi zinapokuja kuwekeza barani humo.

Zitto alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwaka 2012 katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (Unctad), jumla ya uwekezaji wote uliofanyika duniani kwa mwaka jana ni trilioni 1.5 (Dola moja ni sawa na Sh. 1,568) lakini kiasi cha fedha kilichotoroshwa kutoka nchi zinazoendelea kwa mwaka ni wastani wa Dola za Marekani trilioni 0.84 kati yake Dola trilioni 0.58 zilitoroshwa kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kibaya zidi Zitto alisema wakati kiasi cha Dola za Marekani bilioni 538 zinaibwa kutoka Afrika kwa nji za rushwa, ukwepaji wa kodi na mbinu za kutokulipa kodi, ni kiasi cha Dola za Marekani bilioni 80 tu kinaingizwa barani humo kama uwekezaji wa moja kwa moja na misaada.

“Kwa kila Dola moja inayokuja Afrika, Dola nyingine saba zinatoroshwa kutoka Afrika kupitia njia haramu! Hii  haikubaliki,” alisema Zitto katika mkutano huo unaozungmzia pia jinsi kampuni zinavyowajibika kwa jamii kwa kurejesha kila wanachochuma.

Alishauri kuwa uporaji huo ni lazima uzungumziwe kama moja ya ajenda za ushirikiano wa maendeleo baina ya mataifa ya Afrika na yaliyoendelea.

Alisema kwa mujibu wa taarifa kuhusu uadilifu wa matumizi ya fedha duniani ya mwaka jana, kati ya mwaka 2000 hadi 2010, zaidi ya Shilingi trilioni 1,331.8 (Dola za Marekani bilioni 844) ziliporwa  kwa mwaka kutoka nchi zinazoendelea kati yake ya fedha hizo, asilimia 69 zilichukuliwa kutoka nchi za Afrika.

Kwa mfano, Zitto aliuambia mkutano huo nchi kama Uswisi na nyinginezo zenye misamaha ya kodi, zinasaidia sera zake kufanikisha utoroshaji wa fedha kutoka mataifa masikini ya Afrika na pia zinaweka taratibu ngumu za uwazi juu ya fedha hizo hali aliyosema inasaidia kuongeza umasikini Afrika.

Alitaka mataifa rafiki kama Ujerumani kusaidia mataifa ya Afrika katika juhudi za kukataa uporaji unaofanywa na mataifa yenye sera kama za Uswisi.

Zitto aliuambia mkutano huo kwamba Tanzania inaongoza kupokea misaada kutoka nje baada ya Iraq na Afghanistan, lakini bado zaidi ya theluthi moja ya watu wake wanataabika katika umasikini.

“Hali ni hiyo hiyo katika nchi nyingi za Afrika. Mageuzi ya Ushirikiano wa Maendeleo ni yale ya kuwawezesha watu kuamua hatima yao wenyewe," alisema.

Huku akiitaka Ujerumani kuwa mdau na mshirika wa kusaidia mabadiliko ya kimahusiano ya uwekezaji ili mataifa ya Afrika yaamue kuhusu hatma yake yenyewe, alimnukuu hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo akisema:

“Mtu ajiendeleze mwenyewe akikua au akipata kipato cha kujitosheleza na kutunza familia yake. Atakuwa hajaendelea kama atapatiwa vitu hivi na mtu mwingine.”
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment