Siku mbili baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupata pigo la kushindwa rufaa ya ubunge katika Jimbo la Ilemela jijini Mwanza, jana tena kililizwa baada ya Mwenyekiti wake wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, kubwagwa kortini na mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika nafasi ya Udiwani wa Kata ya Kijitonyama Wilaya ya Kionondoni mkoani Dar es Salaam.
Hukumu hiyo imekuja huku makovu ya maumivu kwa CCM yakiwa hayajapona baada ya Mbunge wa Ilemela jijini Mwanza kupitia Chadema, Highness Kiwia, kumbwaga mpinzani wake, Anthony Diallo (CCM) katika nafasi ya ubunge wa jimbo hilo.
Ushindi huo wa Ulole Ulole (Chadema), ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Jaji Upendo Msuya wa Mahakama Kuu.
Jaji Msuya alitamka Ulole ndiye mshindi wa nafasi hiyo iliyogombaniwa mwaka 2010 katika Uchaguzi Mkuu na baadaye Bulembo kwenda mahakamani kupinga.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 uliompatia ushindi Ulole, mpinzani wake, Bulembo alifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupinga matokeo hayo na kufanikiwa kushinda katika kesi hiyo.
Hata hivyo, baada ya Ulole kushindwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alimua kukata rufaa Mahakama Kuu na jana alifanikiwa kuibuka mshindi.
Aidha, Mahakama imemwagiza Bulembo kulipa zaidi ya Sh. milioni 200 za gharama za kesi.
Wakili wa Ulole, Profesa Abdallah Safari, akizungumza na NIPASHE jana alisema hukumu hiyo imempa ushindi mteja wake na Bulembo anatakiwa kulipa gharama zote za kesi.
“Ni kweli tumeshinda kesi iliyodumu kwa zaidi ya miezi sita na mteja wangu Ulole ameshinda na hivyo kumuwezesha kuendelea kuwa Diwani wa Kata ya Kijitonyama,” alisema Profesa Safari.
Hata hivyo, wakati hukumu hiyo inatolewa na mahakama hiyo iliyompa ushindi Ulole, mpinzani wake Bulembo, hakuwapo mahakamani.
Akizungumza na NIPASHE, Ulole alisema kesi hiyo ilikuwa ngumu kiasi cha kumfanya siku ya kuamkia jana ashindwe kupata usingizi.
Alisema anamshukuru Mungu kwa ushindi alioupata.
Ulole alisema mwaka 2010, alishinda kihalali udiwani katika Kata ya Kijitonyama, lakini alishangaa kuona Bulembo akifungua kesi na kuanza kupinga matokeo hayo mahakamani.
Hata hivyo, alisema ushindi alioupata jana ni wa maandishi kwa kuwa hajakabidhiwa kila kitu kutokana na taratibu mbalimbali za kisheria kuwa hazijakamilika.
“Namshukuru Mungu na unyonge wangu hata gari sina, lakini nimefanikiwa kumshinda mtu mwenye nguvu kama huyu kwa kweli namshukuru sana Mungu,” alisema Ulole muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi.
Hata hivyo, Bulembo ambaye alikuwa mkoani Mara kikazi, alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia uamuzi wa mahakama, simu yake ilikuwa imezimwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment