Tuesday, December 4, 2012

''Rwanda Ilisaidia M23 kuteka Goma'' yasema UN

Uwanja wa ndege wa Goma utafunguliwa ili kuwafikishia chakula watu walioachwa bila makao
Ripoti ya Umoja wa mataifa iliyofichuliwa inasema wanajeshi kutoka Rwanda walihusika moja kwa moja na utekaji wa mji wa Goma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliotekelezwa na waasi.
Ripoti hiyo iliyokusanywa kwa ajili ya baraza la usalama, inasema wanajeshi mia tano wa Rwanda, walihusika katika utekaji huo wa kundi la M23.
Msemaji mmoja wa jeshi la Rwanda ameiambia BBC kuwa tuhuma hizo ni za kuudhi na zisizo na msingi.
Wanajeshi wa Congo walirudi Goma hapo jana siku mbili baada ya waasi kuondoka kutoka mji huo wa Goma mwishoni mwa wiki baada ya mkataba wa amani uliofikiwa kwa usaidizi wa nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.
Lakini waasi wameonya kuwa watauteka tena mji huo ikiwa serikali haitatimiza matakwa yao katika muda wa siku mbili.
Waasi hao waliondoka Goma siku kumi na moja baada ya kuuteka mji huo kutoka kwa wanajeshi wa DRC wakiungwa mkono na wanajeshi wa amani wa Umoja wa Mataifa
Mnamo Jumatatu mamia ya wanajeshi wa DRC waliwasili katika kambi zao mjini Goma baada ya waasi kuondoka kutoka mji huo mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini siku ya Jumamosi.
Jean-Marie Runinga (Katikati) ni kiongozi wa kisiasa wa M23
Uwanja wa ndege wa mji huo utafunguliwa Alhamisi ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa huko kuwasaidia mamia ya watu walioachwa bila makao baada ya kutoroka mapigano.
Waasi hao walikubali kusonga umbali wa kilomita 20 kutoka Goma ikiwa serikali itatimiza matakwa yao ikiwemo kuwaachilia wafungwa wa kisiasa. Lakini duru zinseama kuwa wangali wako karibu sana na mji wenyewe kinyume na makubaliano walioafia.
Kuna hofu kuwa hatua yao isidumu ikiwa Rais Joseph Kabila atakataa kuanza mazungumzo nao kulingana na msemaji wa waasi hao kanali Vianney Kazarama.

No comments:

Post a Comment