Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa
Stars imeilaza timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo kwa bao moja kwa
bila katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa katika uwanja wa
taifa mjini Dar es Salaam, Tanzania.
Katika mechi hiyo bao pekee la washindi,
lilipatikana sekunde chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza
likitiwa kimiani na mshambuliaji Mrisho Ngassa.Timu ya Zambia, ambayo ni mabingwa wa Afrika ikiwa pia timu bora ya mwaka barani Afrika na yenye mchezaji bora wa mwaka wa BBC, Christopher Katongo, ilitawala mpira kipindi cha kwanza lakini ikokosa umakini katika umaliziaji.
Kwa upande wa timu ya Tanzania, ambao walionekana kutojiamini katika kipindi hicho, taratibu walibadilika, na kumiliki sehemu ya kiungo.
Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto,Frank Domayo na Salum Abubakar waliichosha ngome ya Zambia kwa kuelekeza mashambulizi mengi, langoni mwa Chipolopolo.
Mrisho Ngassa kama angekuwa makini zaidi angeweza kuipatia timu yake bao la mapema zaidi.
Timu ya Zambia ilichezesha nyota wake wengi akiwemo Christopher Katongo na Stopila Sunzu ambaye anatarajiwa kujiunga na timu ya Reading ya England.
No comments:
Post a Comment