Monday, December 10, 2012

25 mbaroni kwa tuhuma za kuteka gari la maiti Singida

Watu 25 wametiwa mbaroni kwa tuhuma za utekaji gari dogo mali ya Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), kilichopo mkoani Morogoro na kupora abiria mamilioni ya fedha na vitu mbalimbali.


Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Linus Sinzumwa, alikataa kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa maelezo kwamba kufanya hivyo kutaathiri mwenendo wa upelelezi.

Watu hao wanatuhumiwa kuliteka gari dogo aina Toyota Land Cuiser SU 37012 lililokuwa na mwili wa mwanafunzi mwaka wa tatu wa Sua, Munchari Ryoba, uliokuwa ukisafirishwa kwenda Musoma mkoani Mara kwa mazishi.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Kastus Mapulila.

Baada ya majambazi kuliteka gari hilo, walilifungua  jeneza lenye mwili wa marehemu na kufanyia upekuzi.

Tukio hilo la aina yake lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.

Abiria waliokuwa wakiusindikiza mwili huo, waliporwa fedha taslim zaidi ya Sh. milioni 19, zikiwemo za rambirambi na vitu mbalimbali baada ya baadhi yao kushambuliwa kwa mapanga.

Akieleza kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Kamanda Sinzumwa alisema wengi wao ni wakazi wa kijiji cha Kisaki, kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida.

Alisema msako huo unaoendelea pia umefanikisha kupatikana kwa baadhi ya mali zilizoporwa zikiwamo nguo, kamera, laptop na simu za viganjani.

Alisema kukamatwa kwa vitu hivyo kumetokana na ushirikiano wa polisi na wananchi.

Kamanda Sinzumwa alisema baada ya watuhumiwa hao kugawana fedha walizopora, walianza kulewa pombe hovyo huku wakidai hali za uchumi wao zimeimarika.

Alisema baada ya kukamilisha kazi ya upelelezi, ikiwa pamoja na kuchuja kupata washiriki kamili wa tukio hilo, watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment