Friday, December 28, 2012

Mbowe atumia siku nzima kukiokoa Chadema Karatu

KATIKA kile kinachoonyesha kuwa mgogoro na mpasuko kati ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),wilayani Karatu ni ngoma nzito,Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe jana alijifungia siku nzima akifanya vikao vya ndani wilayani humo.
Mbowe aliyewasili Karatu jana asubuhi, alikutana na wajumbe wa kamati ya utendaji wa wilaya ambapo alitarajiwa kutafuta ufumbuzi na suluhu ya mpasuko huo uliosababisha kamati hiyo kusimamishwa kwa muda na Kamati Kuu ya Taifa iliyokutana karibuni jijini Dar es Salaam.
Hakuna kiongozi yeyote wa Chadema wilaya au mkoa aliyekuwa tayari kuzungumzia yaliyojiri kwenye vikao kati yao na mwenyekiti huyo wa Taifa.
“Kikao bado kinaendelea. Siwezi kukueleza lolote kwa sababu ndivyo tulivyokubaliana kutozungumza yanayoendelea hadi taarifa ya pamoja itakapotolewa na viongozi,”alisema mmoja wa viongozi aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya ya Karatu walioomba kutotajwa majina, zimeeleza kuwa pande mbili zinazovutana ziliamua kutumia kikao chao na Mbowe kila upande kuweka mambo yote hadharani ili mbivu na mbichi zijulikane.
“Wenzetu (upande mwingine) walikuwa wanajaribu kuficha udhaifu wao kwenye suala la mradi wa maji kama chanzo cha mtifuano. Sasa tumeamua kueleza ukweli uchungu ambao hawakupenda uelezwe kuwa tatizo hapa ni uongozi mbovu wa halmashauri ya wilaya inayoongozwa na chama chetu,” alisema mjumbe mmoja.
Akifafanua, alisema kinacholeta mgogoro ni baadhi ya viongozi waliokaa madarakani muda mrefu kwenye halmashauri hiyo kulewa madaraka na kuanza kutumia nafasi zao kujineemesha binafsi.
Alisema viongozi hao walioamua kugeuza ugomvi wao binafsi na wananchi wasioridhishwa na matendo yao kuwa suala la kisiasa wanatuhumiwa kujichukulia uamuzi wa
kugawa au kumiliki ardhi bila kujali maslahi ya umma uliowapa fursa ya kuongoza.
Kutokana na uzito wa hoja zilizowasilishwa kwenye kikao kati ya Mbowe na wajumbe wa kamati ya utendaji,
Mwenyekiti huyo alilazimika kufanya kikao kimoja tu badala ya viwili kama ilivyopangwa awali. Jana, Mbowe alipaswa kukutana na kamati ya utendaji pamoja na madiwani kabla ya leo kukutana na wadau wa maendeleo Karatu.

No comments:

Post a Comment