KATIBU mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa amesema chama hicho kinasubiri
kupokea taarifa ya mgogoro unaofukuta ndani ya chama hicho mkoani
Katavi na kusababisha Makamu Mwenyekiti wake Taifa , Said Arfi, kutupa
kadi yake ya uanachama.
Ameeleza kuwa Katiba ya chama hicho
inaeleza wazi kwamba unapoibuka mgogoro, unatakiwa kuripotiwa katika
ofisi ya Katibu Mkuu Taifa ndani ya siku 14.
Tukio la Arfi kutupa
kadi ya Chadema lilikuwa la pili ndani ya wiki moja, kwani juma
lililopita uliibuka mgogoro mwingine wilayani Karatu ambako pamoja na
mambo mengine uliishia kwa Kamati Kuu kuusimamisha uongozi wote wa chama
hicho wilaya.
Arfi ambaye ni Mbunge wa Mpanda Mjini, alitishia
kujitoa Chadema juzi, katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya chama hicho
Mikoa ya Katavi na Rukwa kilichoketi Namanyere, Nkasi na kufikia uamuzi
wa kumsimamisha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoa wa Rukwa, Laurent
Mangweshi.
Katika kikao hicho, Arfi anadaiwa kuichukua kadi yake
ya Chadema na kumtupia Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Rukwa, John Mallack
akitangaza kuachia nyadhifa zote alizonazo, kisha kuondoka ukumbini,
kabla ya kufuatwa na wazee wa chama hicho na kumsihi aichukue kadi yake
hiyo.
Hata hivyo, Mangweshi jana aliliambia Mwananchi kwamba
hajapewa barua hiyo mpaka sasa na kwamba yeye bado ni Mwenyekiti wa
Bavicha mkoa wa Rukwa, kauli ambayo ilipingwa na Katibu wa chama hicho
mkoani Rukwa na Katavi, Ozem Chapita aliyesema kuwa ipo tayari na
wameisafirisha kwa basi jana mchana ili imfikie.
Akizungumzia
tukio hilo jana Dk Slaa alisema taarifa hizo amezisikia ila hawezi
kutoa maamuzi kwa kuwa Chadema kinafuata taratibu za vikao pamoja na
Katiba yake.
“Utaratibu wa chama ni kwamba malalamiko yeyote ni
lazima yawasilishwe katika ofisi ya Katibu Mkuu ndani ya siku 14”
alisema Dk Slaa na kuongeza;
“Mimi kama Katibu Mkuu ni lazima nifuate taratibu za chama na sio kufanya vinginevyo.”
Alisema
kuwa taarifa hizo amezisikia kupitia vyombo vya habari na kwamba
anachokisubiri ni taarifa rasmi ya maandishi ili kama chama kiweze kukaa
vikao na kujadili mgogoro huo.
Alipoulizwa kuna taarifa kwamba
baadhi ya makada wa chama hicho wanatumiwa kukivuruga, Dk Slaa alisema
kuwa inawezekana hilo likawa na ukweli lakini kama kawaida ya chama
hicho, hakitoi maamuzi bila ya kukaa vikao.
“Hizo ni taarifa
ambazo zipo na zinaandikwa kila siku katika vyombo vya habari, zikija
rasmi katika ofisi ya chama zitajadiliwa” alisema Dk Slaa.
Arfi
alifikia hatua hiyo baada ya kutokea sintofahamu kati ya wajumbe wa
kikao hicho katika uamuzi huo uliofikiwa kwa kupiga kura za ndiyo na
hapana.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho
vilifafanua kuwa Arfi alikerwa na kauli iliyotolewa na Mangweshi kuwa
katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alipokea rushwa kutoka kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa kutokana na
hali hiyo, Arfi alipandwa na hasira na kuamua kumrushia kadi Mallack
kisha kutoka nje ya ukumbi.
“Hatua hiyo ilifanya wajumbe wa kikao
hicho nao kutoka nje ya ukumbi na kuanza kumbembeleza ili asichukue
uamuzi huo na kisha wakamwekea kadi yake ya uanachama katika mfuko wake
wa shati,” alisema mmoja wa makada hao.
Arfi mwenyewe hakupatikana juzi kuzungumzia tukio hilo na hata jana alipotafutwa simu zake zote zilikuwa zimezimwa.
Mangweshi aeleza ya moyoni
Akizungumzia kitendo cha kuvuliwa madaraka
Mangweshi alisema mara baada ya kukabidhiwa barua yake atakata rufaa kwa maelezo kuwa haki haikutendeka katika kikao hicho.
Alisema
mpaka sasa taarifa za kuwa amevuliwa uongozi anazisikia katika vyombo
vya habari, huku akisisitiza kuwa yeye bado ni Mwenyekiti wa Bavicha wa
mikoa ya Rukwa na Katavi.
Alipohojiwa juu ya kuonywa mara kadhaa
katika vikao kutokana na utovu wake wa nidhamu alisema, “Katika maisha
yangu sijawahi kuonywa na hata Chadema sikuwahi kuonywa tangu
nilipojiunga mwaka 2001, hakuna kikao cha baraza la uongozi kilichokaa
kunijadili.”
Alifafanua kwamba hata Baraza la Usuluhishi halina
mamlaka ya kumvua mtu madaraka na kuongeza kuwa kikao kilichofanyika
Namanyere kilikuwa ni cha Baraza la Usuruhishi na si cha Baraza la
Uongozi ambalo alidai kuwa ndio lenye mamlaka.
Alisema
ameshangazwa na kitendo cha viongozi wa Chadema mkoani Katavi
kukimbilia katika vyombo vya habari kutoa tamko la kumfukuza kabla ya
kukamilisha taratibu za kichama.
“Mimi ndio nilitakiwa kukimbilia
katika vyombo vya habari kudai haki yangu kama wangenikabidhi barua
yangu, kinyume chake wao ndio wamekimbilia huko tena bila kufuata
taratibu” alisema na kuongeza;
“Kama hawatanitendea haki sitahama
Chadema, nitafia hapa hapa kwa sababu chama hiki lengo lake ni
kulikomboa taifa kutoka mikononi mwa CCM.”
Katibu wa chama hicho
mkoani Rukwa na Katavi, Ozem Chapita alikiri kuchelewa kwa barua ya
kumvua madaraka Mangweshi na kusema kuwa tatizo ni kwamba mwenyekiti
huyo anaishi mkoani Katavi huyu yeye ambaye ni mtendaji mkuu wa chama
hicho akiwa anaishi mkoani Rukwa.
Alisema barua hiyo ipo tayari na wameisafirisha kwa basi ili iweze kumfika Mangweshi.
Tanga kwazidi kufukuta
Katibu
wa Bavicha mkoani Tanga, Deogratius Kisandu ameitaka Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) kubatilisha Uchaguzi Mkuu wa Rais mwaka 2010 kwa kuwa
ulikuwa na wagombea wawili kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema
kitendo hicho kinatakiw akufanywa haraka baada ya Dk Slaa ambaye
aligombea urais mwaka 2010 kwa tiketi ya Chadema kukiri kwama mpaka
sasa bado anayo kadi ya CCM.
“Katika hili ni ni wazi kuwa
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulikuwa batili na kulikuwa na wagombea
wawili kutoka chama kimoja” alisema Kisandu.
Kisandu aliyasema
hayo jana wakati akijibu tuhuma alizotupiwa na Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Tanga, Said Mbweto kwamba amekurupa kutoka tamko la kumtaka Dk
Slaa ajiuzulu.
“Mara baada ya Dk Slaa kukiri kuwa na kadi ya CCM ,
Nec inastahili kubatilisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kuitisha upya
uchaguzi wa Rais ili wajitokeze wagombea wapya wa nafasi hiyo” alisema
Kisandu.
Alisema kwa maana hiyo ni kwamba hata Rais Kikwete kwa
sasa hastahili kuwa katika nafasi hiyo kwa sababu kauli ya DK Slaa
imebatilisha nafasi yake.
Alisema hakukurupuka kutoa kauli hiyo na kwamba yalikuwa mawazo yake binafsi na kusisitiza kuwa msmimamo wake uko palepale.
Karatu wapitisha bajeti
wilayani
Karatu Kamati ya Ushauri ya wilaya ya hiyo (DCC), juzi imepitisha
mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2013/14 ya
Halmashauri ya wilaya hiyo, ambapo kiasi cha Sh 20.6 bilioni
kinatarajiwa kukusanywa.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Clementi
Berege akiwasilisha taarifa ya mapendekezo hayo,katika kikao hicho,
kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Felix Ntebenda, alisema bajeti
hiyo ya 20.6 bilioni ni ongezeko la sh 51.7 milioni ya bajeti iliyopita
ya mwaka 2012/13.
Alisema mapato ya ndani ya halmashauri hiyo
yanatarajiwa kufikia 1.9 bilioni,Ruzuku ya matumizi ya kawaida 17.3
bilioni na ruzuku ya miradi ya maendeleo 2.1 bilioni.
Hata hivyo,
alisema bajeti hiyo, inaweza kubadilika kutokana na maoni na vyombo
vingine vya maamuzi, ikiwepo baraza la madiwani na vyombo vingine kabla
ya kufikishwa kwenye bajeti kuu.
Akichangia taarifa hiyo, Mkuu wa
wilaya hiyo, Ntibenda aliwataka wadau wa maendeleo katika wilaya hiyo,
kuendelea kushirikiana na serikali katika kuifanikisha bajeti hiyo.
Hata
hivyo, Ntibenda aliwataka watendaji na halmashauri na wanasiasa
kushirikiana kwa pamoja kuisaidia wilaya hiyo, kwani wakati wa siasa
umekwisha na kazi iliyombele yao wote ni kusaidia maendeleo ya wakazi wa
wilaya hiyo.
"sitaki kusikia kuna miradi imekwama kwa ajili ya mambo ya siasa, chaguzi zimekwisha sasa tuchape kazi"alisema Ntibenda.
Awali
wajumbe hao pia walipitisha mapendekezo ya kupeleka kwenye kikao cha
kamati ya ushauri cha mkoa wa Arusha(RCC), kuomba barabara ya kutoka
Ayasi-Endabash hadi Manyara kibaoni.
Mkuu wa wilaya hiyo, alisema
barabara hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya wilaya hiyo lakini
halmashauri imeshindwa kuitengeneza kutokana na gharama kubwa kuhitajika
ikiwepo ujenzi wa daraja.
Akizungumza katika kikao hicho, mbunge
wa jimbo la Karatu, Mchungaji Israel Natse, aliwataka watendaji wa
halmashauri ya Karatu kuacha kuwa vikwazo vya maendeleo.
Natse
alisema hivi sasa wilaya hiyo, inakabiliwa na migogoro kadhaa na
kukwama kwa miradi ya maendeleo kutokana na baadhi ya watendaji wa
halmashauri, wakiwepo watendaji wa vijiji kuwavuruga wananchi.
Kikao
hicho, lichofanyika ukumbi ya maendeleo Karatu,pia kilishirikisha
wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya siasa, wakuu wa
idara wa halmashauri ya karatu na viongozi katika ngazi mbali mbali za
wilaya hiyo.
Imeandaliwa Fidelis Butahe, Dar na Juddy Ngonyani, Katavi, Burhani Yakub, Tanga na Mussa Juma, Arusha
No comments:
Post a Comment