RAIS Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa na viongozi wengine wakuu wa vyama
vya siasa nchini wanatarajiwa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya
kuanzia Januari mwakani.
Hayo yalisema juzi Jijini hapa na Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipokuwa akizungumza
na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Arusha wakati
ujumbe wa tume hiyo ulipofika kujitambulisha kwa Mkuu wa Wilaya hiyo,
John Mongela.
Jaji Warioba aliyeungana na ujumbe wa tume
unaokusanya maoni ya wananchi mkoani Arusha tangu Novemba 19, mwaka huu,
aliwataja wengine watakaopata fursa ya kutoa maoni mwakani kuwa ni
viongozi wa taasisi za kidini, vyama vya wafanyakazi, asasi na taasisi
za kiraia.
Kundi lingine litakalotoa maoni mwakani mara baada
ya zoezi la kupata maoni ya wananchi kutoka mikoa yote 30, kukamilika
Desemba 19, mwaka huu ni Baraza la Mawaziri, Makatibu Wakuu wa wizara,
wakuu wa mashirika na taasisi za umma.
Mchakato wa kukusanya maoni kuhusu Katiba Mpya
umegawanyika katika hatua nne ambazo ni kupata maoni ya wananchi wote
kupitia mikutano ya hadhara kila mkoa, wilaya na kata unaotarajiwa
kukamilika Desemba 19, mwaka huu.
Baada ya kukusanya maoni ya wananchi, Tume
itaandaa rasimu ya Katiba Mpya itakayorejeshwa tena kwa wananchi ili
waijadili na kuipitisha.
No comments:
Post a Comment