Monday, December 10, 2012

Butiku awaumbua wanaolilia urais

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amewashushua wanasiasa vijana kuachana na propaganda za kupigania nafasi za kisiasa na badala yake wafanyekazi kwa bidii na maarifa ili waonekane kuwa wanafaa kuwa viongozi.

Butiku aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye kongamano la Uhuru lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), lililokuwa na kaulimbiu ya ‘Uhuru wetu na Mustakabali na Taifa letu kwa miaka 50 ijayo’.

Alisema wakati umefika wa kupunguza maneno na kutumia muda mrefu kujadili mipango ya kazi badala ya porojo za maneno ya kutafuta nafasi ya urais kama ilivyo hivi sasa.

Butiku aliyasema hayo akionekana kama anamjibu Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, ambaye awali alisema nyakati za kuwa na marais waliozaliwa kabla mwaka 1961, zimepita na kutaka vijana wapewe nafasi.

“Fanya kazi wenzako waone kwamba unafaa kuwa kiongozi wa nchi, acheni propaganda za kuwa marais, mawaziri au wabunge na badala yake msimamie kwenye misingi ya Taifa iliyoasisiwa na wazee wa Taifa hili,” alisema Butiku.

Alisema waasisi wa Taifa walifanyakazi ambayo inaonekana katika maeneo ya uhuru, elimu, maliasili na nyanja nyingine na ndiyo maana Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alihakikisha rasilimali za nchi hazitumiki vibaya.

Alisema nia ya Mwalimu Nyerere ilikuwa njema ili zitumiwe na Watanzania pindi watakapokuwa na elimu ya kuzisimamia.

Alisema mategemeo ya kutochezea rasilimali hizo ilikuwa kuviachia vyuo vikuu kama cha Dar es Salaam kizalishe wataalamu hao.

“La kujiuliza ni kwamba, mali inavyochimbwa sasa hivi na mataifa ya nje yakishiriki kufanya hiyo kazi, wako wapi Watanzania waliotakiwa kuzalishwa na vyuo hivi? Mbona hawaonekani kuzisimamia rasilimali hizi?” Alihoji Butiku.

Alisema umefika wakati kwa vyuo vikuu kutengeneza mitaala itakayowaelimisha Watanzania na wataalamu wengine katika kutekeleza misingi ya Taifa ambayo ilijali watu kwanza ambao walipewa mamlaka ya kuamua matumizi ya rasilimali za nchi.

Hata hivyo, hotuba hiyo ya Butiku ilionekana kulenga kumjibu Makamba ambaye awali alitaka wazee kuwapa nafasi vijana kwa kuwa wana uwezo wa kuiongoza nchi.

Makamba ambaye alizungumza kabla ya Butiku, alisema nyakati za vijana kuendesha siasa za nchi zimefika kwa kuwa wana elimu na maarifa ya kukabiliana na changamoto za kuivusha nchi kwenda kwenye miaka 50 ijayo yenye neema.

Hata hivyo, alikumbusha umuhimu wa kuitazama nafasi ya urais kama taasisi badala ya kuangalia majina ya watu wanaonyesha nia ya kuwania kiti hicho.

 Alisema kwa kuangalia majina, Watanzania wanasahau changamoto zilizopo ambazo zinapaswa kushughuliwa na taasisi ya urais.

“Hatufikirii kiongozi kama masiha, ila jamii nzima, ndiyo maana ninahimiza umuhimu wa kuachana na siasa za kuangalia majina kwa kuwa hazitatusaidia katika miaka 50 ijayo,” alisema.

Hata hivyo, alisema amani na utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi lakini haki, usawa na siasa za nchi ni vihatarishi vya amani.

Alisema serikali na mamlaka mbalimbali zinapaswa kutoa huduma kwa haki ikiwamo haki ya elimu na afya ili kuepuka chokochoko za kuvunja amani.

Alisema ili kumkomboa Mtanzania, ni lazima fursa za kupata elimu zitolewe kwa usawa kwa wananchi wote na mtoto wa mkulima wa kawaida apate elimu sawa na wa kiongozi yeyote wa nchi.

Kwa upande wake, Dk. Haji Semboja wa UDSM, ambaye alikuwa mtoa mada kwenye kongamano hilo, alisema ili nchi ipige hatua haraka, ni vyema mkazo ukawekwa kwenye sekta za kitaifa zinazosimamia rasilimali za nchi kama Shirika na Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Shirika la Madini (Stamico).

Alisema sera na sheria za sekta kama za madini, hazitaleta manufaa stahiki kwa Taifa kama mashirika hayo hayatakuwa na nguvu.

Alitoa mfano kwamba pamoja na kuboresha sheria na sera za madini, mchango wa madini katika pato la Taifa umeshuka kutoka asilimia 10 hadi moja.

Kwa upande wake, Mshauri wa wanafunzi katika Chuo Kikuu Kkishiriki cha Elimu (Duce) ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk. Kitila Mkumbo, alizungumzia umuhimu wa kuboresha maslahi ya walimu ili kunusuru kiwango cha elimu kilichoporomoka.

Alisema katika miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2009, kiwango cha wanafunzi wanaofeli kidato cha nne kimefikia asilimia 80 na hali hiyo inasababishwa na kutowekeza katika maslahi ya walimu.

Mwanazuoni na Mwanasheria mashuhuri nchini, Profesa Issa Shivji, alisema Tanzania imegawanyika katika mataifa mawili ambayo ni maskini wengi na matajiri wachache na ni wakati sasa wa kudhibiti hali hiyo.

Wasomi na wananchi mbalimbali walieleza umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu na fursa sawa za matumizi ya rasilimali za Taifa.

Akifunga kongamano hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema ili Tanzania isonge mbele kwa miaka mingine 50 ijayo ikiwa kwenye amani na utulivu, inahitaji viongozi wenye mkakati, maono na uadilifu ambao watapambana na changamoto za nchi kama ukosefu wa ajira na kuhimili ongezeko la watu kulingana na rasilimali zilizopo.

Alisema takwimu zinaonyesha kwamba miaka 13 ijayo, Tanzania itakuwa na watu milioni 65 na hivyo akatoa changamoto kwa wasomi kutumia weledi wao kufanya tafiti ili kuwashauri wanasiasa wazifanyie kazi na kufikia malengo ya taifa.

Alisema bila utafiti hakuna maendeleo na hiyo ndiyo zana pekee ya kushindana kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment