SIKU chache bada ya Baraza la Vijana wa Chadema Mkoa wa Mwanza
kutamka kuwa hawako tayari kuunga mkono maandamano ya kumpinga Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa,
Bavicha Mkoa wa Singida, wameibuka na kuwaunga
mkono wenzao wa Mwanza kwa kusema kuwa watasimama nyuma ya Katibu Mkuu
huyo hadi mwisho wa mapambano.
Kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya
habari na Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Singida, Josephat Isango, vijana
hao wameeleza kusikitishwa kwao na wenzao wanaompinga Dk Slaa, huku
wakidai kuwa wenzao hao wanatumiwa na wanasiasa wa upande wa CCM.
Walidai kuwa huo ni utekelezaji wa propaganda kutoka Idara ya Uenezi ya CCM.
Walidai kuwa huo ni utekelezaji wa propaganda kutoka Idara ya Uenezi ya CCM.
Katika siku za karibuni vyombo vya habari
viliripoti hatua iliyoelezwa kuwa ya Bavicha, kumshinikiza Dk Slaa
kuachia ngazi kwa madai ya kumiliki kadi ya CCM, madai yaliyotolewa na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Isango katika taarifa hiyo ya jana alidai kuwa,
baadhi ya vijana waliofukuzwa na Chadema kutokana na utovu wa nidhamu,
ndiyo wamekuwa wakiendeleza mapambano hayo ili kukichafua Chadema,
kionekane kuwa na migogoro wakati ukweli ni kwamba hakuna hali hiyo.
Alisema kuwa Vijana wa Singida walifanya uchunguzi
na wabaini kuwa baadhi ya vijana wenzao ndiyo wanaotumiwa na Nape kwa
masilahi ya CCM.
Kutokana na hilo, Isango alimtaka Nape kuachana na
kile alichokiita kuwa ni siasa za maji taka, akieleza kuwa siasa hizo
zinalenga kuwarubuni na kuwaaminisha Watanzania kuwa CCM peke ndicho
chama bora wakati siyo kweli.
“Hata hivyo, vijana waliosimamishwa uongozi ndani
ya Chadema ni vyema wakajiunga na CCM wazi ili wakasaidie mafisadi
waliosababisha maisha magumu kwa Watanzania. Watanzania wanajua hali yao
ya maisha na ndiyo waamuzi sahihi wa Tanzania wanayoitaka, tusiwalishe
maneno ya uongo kurutubisha ufisadi nchini,” alisema.
Isango aliongeza: “Ni imani yetu kuwa, kila jambo
linalofanywa ndani ya Chadema linakuwa na baraka njema kwa ajili ya
ukombozi wa nchi yetu, lakini yako yanayofanywa kwa mashinikizo mabaya
kama hili hayana nia njema kwetu.”
Mwenyekiti huyo aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa
ngazi za juu ndani ya CCM kuwa wamekuwa wakitumika kwa ajili ya
kukisambaratisha Chadema kwa mashinikizo yao binafsi na kwamba watu hao
wanatamani kuona siku moja Chadema kikisambaratika.
No comments:
Post a Comment