CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Kenya,
kimezungumzia uamuzi wake wa kumwalika Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni nchini humo, uliozua
mjadala mkubwa nchini.
Desemba 7 mwaka huu, chama hicho cha upinzani nchini Kenya kilimwalika Dk Magufuli kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja vya Kasarani ambako pamoja na mambo mengine, alimpigia debe Raila Odinga ili achaguliwe kuwa Rais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Machi mwakani.
Hatua hiyo ya Dk Magufuli ilizua mjadala mkubwa, huku Chadema kikidai kuwa ni makosa kwa nchi moja kuingilia siasa za nchi nyingine na kumtaka waziri huyo aeleze kama alitumwa na Serikali au la.
Chadema pia kilimtaka Rais Jakaya Kikwete atolee kauli hatua hiyo ya waziri wake, vinginevyo nchi itakuwa na uhusiano mbaya na Kenya, endapo Raila hatachaguliwa kuwa Rais.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa ODM, Profesa Peter Anyang’Nyong’ alisema hakuna haja ya Watanzania kumzonga Waziri Magufuli, kwani ujio wake Kenya, ulitokana na mwaliko wa Odinga.
Profesa Anyang’Nyong’ ambaye chama chake cha ODM kilitangaza kuungana na chama kingine cha Wiper Democratic cha Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka katika uchaguzi huo alisema Odinga alimwalika Magufuli kama rafiki yake wa muda mrefu na rafiki wa ODM.
“Waziri Mkuu wetu Odinga ndiye aliyemwalika Magufuli na alimwalika kama rafiki yake wa karibu. Kuja kwake huku (Kenya) kulikuwa safari binafsi. Hakukuwa (kuja) na uhusiano wowote na wadhifa alio nao Tanzania,” alisema Profesa Onyang’Nyong’.
Alisema ziara ya Magufuli iliratibiwa na Odinga ambaye aligharimia kila kitu na kwamba mwaliko huo ulifanywa kwa kuzingatia ushirikiano wa muda mrefu baina yao.
Profesa Anyang’Nyong’ alisema ODM kumwalika Dk Mafuguli ni mwendelezo wa uhusiano wa wanasiasa wa Tanzania na Kenya uliokuwapo tangu enzi za viongozi; Jomo Kenyatta, Tom Mboya na Mwalimu Julius Nyerere ambao walifanya pamoja kazi ya kudai uhuru.
“Kizazi cha sasa lazima kitambue ushujaa wa viongozi wetu wa zamani ambao walituonyesha namna wanavyoweza kufanya siasa kwa pamoja na kufanikisha malengo yao,” alisema na kuongeza:
“Mambo kama haya lazima tuyatambue kwani sisi sote ni wamoja tena tuna shabaha ya kuwatumikia wananchi wetu. Tunapopata viongozi wenye mitazamo inayofanana kama ile ya waasisi wa mataifa yetu lazima tuwaunge mkono na kuwapa fursa.
“Kwetu sisi Magufuli tunamwona kama shujaa tena mtu ambaye anaweza kutoa idea (mawazo) yanayoweza kukusaidia kusonga mbele kwenye siasa.”
Alisema Dk Magufuli ana uzoefu mkubwa na mambo ya siasa na ODM wanatambua umuhimu wake katika siasa zao.
Alipuuza madai kwamba kumwalika Dk Magufuli ni kuingilia siasa za Kenya na huenda hatua hiyo ikadhoofisha uhusiano wa kidiplomasia… “ Kuja kwake hakumaanishi kwamba ameingilia mambo ya Kenya au siasa za taifa hili…. Huyu ni rafiki yetu na alikuwa kama mtu wetu wa karibu.”
No comments:
Post a Comment