MIONGONI mwa mambo yatakayokumbukwa katika kesi iliyotengua na baadaye
kumrejeshea ubunge, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ni mawakili wa
pande mbili zilizokuwa zikipambana katika kesi hiyo ya kuhistoria.
Kwanza
ni mawakili ndugu; Tundu Lissu ambaye alikuwa akimtetea Lema na Alute
Mughway ambaye alikuwa wakili wa makada wa CCM waliofungua kesi kupinga
ushindi wa Lema.
Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakili mwenzake, Method Kimomogolo
walishirikiana kumtetea Lema ambaye ni kada wa Chadema.
Lakini
kaka yake (Mughway) alikuwa anawatetea warufaniwa (wajibu rufaa) ambao
ni makada wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.
Alute
na Tundu wote ni watoto wa Mzee Augustino Lissu Mughwai na Bibi Alu
Alute Tundu ambao wote sasa marehemu. Wakati Alute ni mzaliwa wa pili
katika familia hiyo ya watoto 12, Tundu ni mzaliwa wa tano.
Alute
hivi sasa ni wakili wa kujitegemea akifanyika kazi zake mkoani Arusha
wakati mdogo wake Tundu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki ni
wakili akifanyia kazi zake jijini Dar es Salaam.
Ndugu hawa
walikuwa kivutio katika kesi hiyo kwani wote walionekana kuwa mahiri
katika kujenga na kupangua hoja pale walipokuwa wakiishawishi mahakama
kuwapa ushindi wateja wao.
Ndugu hawa wawili wamekuwa wakipambana
mahakamani kwenye kesi ya Lema tangu ifunguliwe Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010.
Hukumu ya kesi hiyo ndiyo iliyomvua ubunge Aprili 5,
2012 lakini Lissu na wakili mwenzake Method Kimomogolo awalikata rufaa
ambayo jana ilimrejeshea Lema Ubunge.
Hii inatoa picha kwamba
katika fani ya ya sheria hasa kwenye uwakili mahakamani huweza
kuwakutanisha maadui kutoka pande mbili, mtu na mwanaye katika pande
hizo mbili lakini kila mmoja akisimamia kile anachokiamini ili kufanya
kazi yake.
Baba anaweza kuwa upande wa utetezi na mtoto anaweza
kuwa upande wa mashtaka, kila mmoja akitaka kuonyesha uwezo wake kwa
mteja wake.
Wakati mwingine watu huweza kusema kwa nini huyu
asizungumze na mwanaye ili asitoe hoja nzito au mtoto asizungumze na
baba yake ili asitoe hoja nzito ili kurahisisha kesi. Lakini hayo hayana
nafasi pale watu hawa wanapokuwa katika kazi zao hasa za kitaaluma.
No comments:
Post a Comment