ASILIMIA 44 ya wapenzi wanaokwenda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali kupima vinasaba (DNA), kwa ajili ya kujua uhalali wa watoto kwa
baba, wamethibitishiwa kuwa watoto hao si wa kwao.
Takwimu za mwaka 2012 kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu
wa Serikali, zimeainisha kuwa kati ya watu 90 waliokwenda kupima DNA, 40
ambao ni sawa na asilimia 44, wameonekana kubambikiziwa watoto.
Takwimu hizo za kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka
huu, zilionyesha kuwa katika kesi 50 za waliokwenda kupima, matokeo
yalionyesha kuwa ni wazazi halisi wa watoto wao.
Hata hivyo, idadi hiyo inayoonyesha kuwa kinababa
siyo wazazi halisi wa watoto, imeshuka ikilinganishwa na takwimu za
mwaka 2008/2009 ambazo zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watu waliochukua
vipimo hivyo wamebainika kuwa si wazazi halisi wa watoto hao.
Mkemia na Mtambuzi wa Vinasaba vya Makosa ya
Jinai, Gloria Machuve alisema jana kuwa ni vyema ikitambulika kwamba
takwimu hizo zinatokana na watu waliokwenda kupima baada ya kutokea
migogoro ya kimapenzi na siyo takwimu iliyochukuliwa kutoka kwa
Watanzania wote.
“Hatusemi kuwa sasa wanaume wote Tanzania wanalea
watoto ambao si wa kwao. Hizi ni takwimu za waliokuja kupima; yaani
wale wenye matatizo,” alisema.
Machuve alisema katika maabara hiyo, kesi nyingi
zinazoonyesha kuwa watoto hao si halali, zimetokana na uhusiano wa ziada
au usio rasmi baina ya wenza.
“Kwa mfano, mwanamume ana mwanamke wa nje ya ndoa
au mwenye uhusiano usio rasmi, halafu mwanamke huyo anadai mtoto ni wa
huyo mwanamume, mara nyingi matokeo huwa si mazuri,” alisema Machuve.
Aidha, Machuve alisema takwimu za kuanzia mwaka
2005 hadi 2010 zinaonyesha kuwa tabia ya upimaji imeongezeka miongoni
mwa Watanzania.
Alisema mwaka 2005/2006, kesi za upimaji wa
vinasaba zilikuwa 96 na mwaka 2008/2009 kesi hizo zilikuwa 113 wakati
mwaka 2009/2010, kesi za waliokwenda kupima zilifikia 125.
Alisema watu wengi wanaojitokeza kupima katika
miaka ya karibuni wanataka kufahamu uhalali wa watoto wao ili wawajibike
kuwalea kihalali.
No comments:
Post a Comment