Katika hatua nyingine, suala la ufisadi ndani ya CCM limeendelea
kutikisa chama hicho, baada ya wajumbe wa mkutano mkuu kupendekeza kuwa
makada wanaotuhumiwa kwa kashfa hiyo wavuliwe uanachama.
Vilevile,
wanachama hao wamependekeza viongozi wanaotoa hadharani siri za Baraza
la Mawaziri na kuikosoa hadharani Serikali waadhibiwe, wakieleza kuwa
matendo hayo yanakiuka maadili ya kazi zao.
Wakitoa maazimio
yaliyopatikana kutoka katika makundi yaliyokuwa yakijadili taarifa ya
utekelezaji wa Ilani ya CCM, iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa chama
hicho, Wilson Mukama na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi mchana, wajumbe
hao walisema kuendelea kuwapo ndani ya chama hicho watu hao
kunahatarisha usalama.
Akiwasilisha mapendekezo ya kundi la tatu,
lililokuwa la Mikoa ya Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Tanga, Rukwa na
Mjini Magharibi, Dk Damas Mkasa katika kundi lao wamependekeza makada wa
CCM ambao wamekuwa wakikivuruga kwa kuendelea kupandikiza mpasuko
waondoke.
“Wenye ndimi mbili wanaotengeneza migogoro ndani ya
chama chetu waondolewe, ili CCM iendelee kushika hatamu ya nchi,”
alisema Dk Mkasa, huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano ukumbi mzima.
Emmanuel
Lwegenyeza akiwasilisha mapendekezo ya Mikoa ya Kigoma, Dar es Salaam,
Kusini Unguja, Geita, Manyara na Shinyanga, alisema wajumbe katika kundi
hilo wametaka wanachama wa CCM wanaotuhumiwa kwa kujihusisha na rushwa
waondolewe.
“Wale ambao wanajihusisha na rushwa ndani ya chama wafukuzwe,” alisema.
Awali
juzi jioni, wakichangia katika makundi wajumbe kutoka Mikoa ya Arusha,
Tabora, Singida, Kusini Magharibi na Ruvuma, ambao walikuwa katika
Ukumbi wa Kizota, kama wazee ndani ya chama hicho, walishindwa
kuwadhibiti waachie ngazi na kuwakabidhi majukumu hayo vijana.
Mbunge
wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala alisema, haiwezekani wazee waendelee
kuitafuna nchi, huku Watanzania wakiendelea kuwa maskini.
“Haiwezekani wazee waendelee kuitafuna nchi na kujinufaisha wao wenyewe, kama wamechoka waondoke,” alisema.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, mbunge huyo alishangaa
kuona ndani ya chama hicho kuna makanda wanaotuhumiwa kwa ufisadi,
lakini wamekuwa wakijitetea kuwa wasafi, huku wakiendelea kukigawa
chama.
Mwakilishi wa kundi namba nne, Balozi Ali Mchumo
alipendekeza kuwa ni wakati mwafaka kwa CCM kuwafagia watu wote ambao
wamekuwa wakikihangaisha chama na kuwafanya wajumbe kuwa na makundi.
“Wanaomomonyoa
chama watoswe kwa faida ya wengi, tumependekeza hata wale wanaovujisha
siri za chama watoswe pia kuliko kuendelea kuwa nao,” alisema Mchumo.
Charles
Mwakipesile ambaye alikuwa ni mwakilishi wa kundi namba tano
alipendekeza kuwa watu wote ambao wamekuwa ni tatizo ndani ya chama
waanze kwa kuonywa na wakirudia tena ndipo wafukuzwe.
Mwakipesile
alisema ili chama kionekana kuwa ni bora, hakina budi kujipambanua kwa
kuwafukuza pale itakapobidi wale ambao wanakipaka matope chama hicho.
No comments:
Post a Comment