Sunday, November 18, 2012

UZINDUZI WA MASHUJAA: JB Mpiana kutua Nov. 26

MWANAMUZIKI nguli wa dansi barani Afrika, JB Mpiana, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anatarajiwa kuwasili nchini Novemba 26, kwa ajili ya kupamba uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band itakayozinduliwa kwenye viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam Novemba 30, mwaka huu.
Kabla ya kufanya shoo jijini Dar es Salaam, JB Mpiana atatumbuiza katika ukumbi wa Tripple A jijini Arusha Novemba 28, kabla ya kuhamia jijini Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park, Desemba 2.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, Rais wa Mashujaa Band, Charles Gabriel ‘Chalz Baba’, alisema mkali huyo wa dansi kutoka Congo, anakuja na kundi lake zima la Wenge Musica BCBG.
Alisema JB Mpiana ambaye kwa sasa anatamba na albamu yake mpya iitwayo Biloko, anatarajiwa kupagawisha Watanzania na rapu yake mpya iitwayo ‘Amataka na Punda’ yaani Panda Punda, ambayo kwa Congo ni gumzo hivi sasa.
Chalz Baba alisema, maandalizi ya onesho lao yanaendelea vizuri kwa ujumla na wanamuziki wako tayari kuwapa raha Watanzania siku hiyo, huku wakitarajia kuingia kambini wiki hii nje kidogo ya jiji.
Alisema albamu yao wanayozindua iitwayo ‘Risasi Kidole’ ina nyimbo sita, ambazo ni ‘Risasi Kidole’ yenyewe ikiwa ni utunzi wake mwenyewe: ‘Ungenieleza’ kazi ya Raja Ladha, ‘Umeninyima’ wa Freddy Masimango, na ‘Hukumu ya Mnafiki’ utunzi wake Jado FFU.
Nyingine ni ‘Kwa Mkweo’ utunzi wake Baba Isaya na ‘Penzi la Mvutano’, ambao umetungwa na Masoud Namba ya Mwisho.
Alisema kama ilivyopangwa, mbali na JB Mpiana, wanamuziki wengine watakaopamba uzinduzi huo ni MB Dogg, H. Baba, Ney wa Mitego na wengineo ambao watajulikana baadaye.
“Sisi kwa upande wetu, tumejipanga vizuri kuwapa watu burudani, ambayo tunajua kwa muda mrefu wameikosa Mashujaa tunakuja kishujaa, ushujaa wa kuwaburudisha watu na kukata kabisa kiu yao,” alisema.
Hadi sasa wapenzi wa muziki hapa Dar es Salaam, ambao wamebahatika kuona shoo zetu, wanakiri sisi ndio mabingwa wapya wa muziki wa dansi Tanzania, sasa tunataka tumdhihirishie hilo na JB Mpiana.
Uzinduzi huo, umeandaliwa na kampuni ya Qs Mhonda, kupitia kwa Mkurugenzi wake Joseph Mhonda, ambaye amesisitiza kuwa kila kitu kiko sawa na kinachosubiriwa ni JB Mpiana kutua kwa ajili ya shoo hiyo tu.
Naye wakala wa JB Mpiana, Guyguy Kiangala, amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo na kuona ubora wa JB Mpiana akichuana na Mashujaa.

No comments:

Post a Comment