Thursday, November 22, 2012

Askari waliohukumiwa kifo kukata rufaa

SIKU moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwahukumu adhabu ya kifo askari wa wiwili wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mmoja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Swetu Fundikira, wafungwa hao jana wamewasilisha hati mahakamani hapo ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Wafungwa hao ni MT 1900 Sajenti Roda Robert (42), MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa kikosi cha JWTZ Kunduchi.
Wakili wa askari wa wafungwa hao, Mluge Karoli, alisema ameishawasilisha hati hiyo mahakamani hapo jana kwa madai kuwa wateja wake hawakubaliani na hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Zainabu Mruke ambaye aliwatia hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Karoli alieleza kuwa sababu zilizomsukuma yeye na wateja wake kuwasilisha hati hiyo ni kwamba  kesi yoyote ya ugomvi  haiwezi  kuwa na kusudio la kutaka kuua na kwamba hakuna shahidi wa upande wa jamhuri aliyefika mahakamani hapo na kueleza kuwa wateja wake ndiyo wamemuua Swetu Fundikira.
Alieleza kuwa, aliyepambana na wateja wake ni Swetu Fundikira na uchunguzi wa daktari unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira hivyo ni watu wawili tofauti, na kwamba hakuna hata shahidi mmoja alifika mahakamani na kueleza aliwahi kuuona mwili wa marehemu au kuhudhuria kwenye msiba.
Askari hao kwa pamoja walidaiwa kuwa walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku huo huo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akisoma hukumu hiyo juzi , Jaji Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na  upande wa mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka hayo.

No comments:

Post a Comment