Thursday, November 22, 2012

Mahakimu 370 wanalipwa mamilioni bila kufanya kazi

UKOSEFU wa umakini serikalini, umeendelea kuliingiza taifa kwenye gharama zisizo za msingi ambapo sasa mahakimu wakazi 370 wanalazimika kulipwa mishahara bila kufanya kazi, Tanzania Daima limebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa mahakimu wakazi 300 waliajiriwa Juni mwaka huu katika ajira mpya kwa masharti kwamba wangefanya kazi kwenye mahakama za mwanzo.
Baadaye Septemba mwaka huu, mahakimu wengine 70 waliapishwa na kupandishwa kutoka mahakama ya mwanzo kuwa mahakimu wakazi na hivyo kufanya idadi yao kufika 370 ambao hulipwa takribani sh 700,000 kila mmoja kwa mwezi.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kama kukosekana kwa umakini katika utendaji serikalini, sheria iliyopo sasa kuhusu utendaji wa mahakimu hao ilipaswa kufanyiwa marekebisho kwanza kabla ya wao kuajiriwa.
Kwa mujibu wa sheria ya sasa ya mahakimu na mahakama sura namba 11 kifungu cha sita, ni kwamba hakimu mkazi hana mamlaka ya kukaa katika mahakama ya mwanzo bali mahakama ya wilaya na ya hakimu mkazi (mkoa).
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya mahakimu hao waliilalamikia serikali kwa kukurupuka kuwapa ajira bila kufanyia marekebisho sheria, na hivyo kuhoji ni kwanini wasipangiwe kazi kwenye mahakama zenye hadhi yao hadi sheria itakapokuwa imebadilishwa.
“Kwa kweli kitendo hiki cha kulipwa mshahara pasipo kufanya kazi ni kama kuhujumu uchumi wa nchi, lakini pia serikali imeamua kuharibu taaluma zetu,” kilisema chanzo chetu.
Kwa sasa mahakimu hao wanaripoti tu kwenye vituo vyao vya kazi na kusaini kitabu cha mahudhurio kisha kuondoka kwa vile hawana kazi maalumu ya kufanya katika mahakama hizo.
“Mikoa kadhaa kama Mwanza na Pwani, majaji wenye uelewa wanawapangia kazi mahakimu hawa kwenye mahakama stahiki. Lakini bado si maeneo yote wanafanya hivyo.
“Serikali ni kweli ilikuwa na nia njema ya kuboresha mfumo wa mahakama ili hawa wasomi wahudumie huko, lakini kwanini wasirekebishe sheria kwanza?” kiliongeza chanzo hicho.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe pamoja na Naibu wake, Angela Kairuki hawakuwa tayari kupokea simu na hata walipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno vile vile hawakujibu, hivyo juhudi za kuwatafuta ili wafafanue zinaendelea.
chanzo-Tanzania daima

No comments:

Post a Comment