Tuesday, November 20, 2012

Kigoda: viwanda vinaweza kuinua uchumi

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda  amesema ni wakati wa kutochukulia kwa mazoea dhana iliyojengeka kuwa Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, bali hata viwanda vina nafasi yake kwa kuwa nchi mbalimbali zilizoendelea  zinategemea  viwanda.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa  ripoti ya ushindani wa Viwanda (Tanzania Industrial Competitive) uliofanyika  Dar es Salaam jana.

Kigoda alisema ni wakati wa kugeuza fikra  kwa  kuisaidia sekta ya viwanda na  kuwataka wadau wajenge viwanda, na waache  kusema kuwa kilimo ndio pekee  uti wa mgongo wa taifa.

“Mageuzi ya fikra zetu  yanahitajika  wakati huu ili tuweze kuleta maendeleo katika nchi yetu, ni lazima tuachane na dhana ya mazoea kwamba uti wa mgongo wa taifa letu ni kilimo pekee, badala yake tuangalie na sekta nyingine kama viwanda  kwani nchi nyingi zilizoendelea zimejikita kwenye viwanda pia,” alisema
 Kigoda.
Alieleza kuwa  ripoti hiyo   imejikita zaidi kutatua   changamoto mbalimbali inayoikumba  sekta hiyo ikiwemo  serikali kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji,  ubora wa miundo mbinu  pamoja na utawala wa kuchukia rushwa na urasimu.
Alisisitiza kuwa kiwango cha biashara katika nchi nyingi za  Afrika ni kidogo kulingana na nchi nyingine duniani na kwamba ni 10% kumi tu ya biashara inayofanyika baina ya nchi za Afrika ukilinganisha na nchi ambazo zimeendelea.

 Kwa mujibu wa Kigoda  katika nchi za Afrika  hakuna masoko ya ndani kwa ajili ya kuuza bidhaa,  vilevile kuna vikwazo vya biashara  na ukosefu wa mtaji fedha jambo ambalo linasababisha  kudorora kwa biashara katika masoko ya Afrika.

“Nchi za Afrika zinakabiliwa na ukosefu wa masoko ya ndani, halafu zina vikwazo vingi  vya kuendesha biashara na ukosefu wa mtaji  kwa ajili ya kuanzisha viwanda jambo ambalo linasababisha kuzorota kwa  biashara  Afrika,” alisema Kigoda.
 Pia alifafanua  ni lazima  Serikali na sekta binafsi  iondokane na dhana ya nadharia na kufanya vitendo  kwa  ajili ya kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

“kama tunataka kukuza uchumi wa nchi yetu lazima tuondokane na dhana ya  kufanya mambo kwa nadharia, badala yake tujikite kwenye vitendo ili tukuze na kuinua uchumi wa nchi yetu, hili litafanikiwa kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi”, alisema Kigoda.
 Mmoja wa waandaji wa ripoti hiyo, Falecia Massak alisema ripoti hiyo  imeonesha  kuwa  katika  Tanzania viwanda haviwezi kutengeneza  ajira ya kutosha kwani hakuna viwanda  vikubwa, na vilevile havijasambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Massak alisema viwanda vingi vipo katika jiji la Dar es Salaam na vichache  Arusha, jambo ambalo linasababisha kutokuwa na ajira ya kutosha kwani Tanzania ina miji mingi.

No comments:

Post a Comment