Sunday, November 18, 2012

Serengeti Boys yajiweka pabaya NI BAADA YA USHINDI MWEMBAMBA.

TIMU ya soka ya taifa Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa umri huo baada ya jana kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Congo Brazaville.
Katika mechi hiyo ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazopigwa mwakani nchini Morocco, iliyopigwa kwenye dimba la Taifa, jijini Dar es Salaam, Serengeti ilijipatia bao hilo la pekee dakika ya 16, likitiwa kambani na Mudathiri Abbas kwa shuti kali nje ya 18, baada ya Joseph Kubasha kuchezewa vibaya na beki mmoja wa Congo Brazaville.
Serengeti iliendelea kutengeneza nafasi kadhaa, lakini kukosekana kwa umakini kulifanya hadi mapumziko kutoka na bao hilo moja.
Kipindi cha pili, timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu.
Dakika ya 60, mwamuzi alimwita Kocha wa Congo, Eddie Hudanski, na kuzozana naye baada ya kocha huyo kuzozana na kamisaa akipinga faulo ya kuotea iliyoonyeshwa na mwamuzi wa pembeni.
Dakika ya 80, mwamuzi huyo uzalendo ulimshinda na kumtimua kocha huyo uwanjani, baada ya awali kumpa onyo kutokana na kuzonazana naye.
Katika mechi hiyo, mashabiki walijitahidi kiasi kujitokeza kuwapa sapoti Serengeti Boys huku kikundi cha ushangiliaji cha Azam FC kikiwa pekee mstari wa mbele mwanzo-mwisho kuwapa nguvu makinda hao wa U-17.
Kwa ushindi huo, Serengeti inayonolewa na Mdenish Jakob Michelsen na Jamhuri Kihwelo ‘Julio Alberto’ italazimika kulazimisha sare ya aina yoyote wiki mbili zijazo ugenini, ili kukata tiketi ya kwenda Morocco mwakani.
Serengeti Boys: Peter Manyika, Niza Abdallah, Mohammed Hussein, Ismail Gambo, Miraji Seleman, Mudathir Abbas, Mohamed Haroub, Joseph Kubasha/Dickson Ambundo, Hussein Ibrahim ‘Messi’, Seleman Bofu/Tumaini Mosha, Farid Shah.

No comments:

Post a Comment