Friday, November 30, 2012

Bakwata yamkana Sheikh Ponda mahakamani

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limemkana Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake, baada ya kudai mahakamani kuwa eneo walilovamia wakidai ni mali ya Waislamu linamilikiwa kihalali na kampuni ya Agritanza.
 

Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila alisema hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya jinai inayomkabili Ponda na wenzake 49 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa pamoja na mambo mengine kuvamia na kupora ardhi na wizi wa vifaa vya ujenzi.

Akitoa ushahidi wake jana huku akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, Lolila ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka alidai kuwa eneo hilo awali lilikuwa likimilikiwa kihalali na Bakwata.

Hata hivyo, alidai kuwa baadaye Bakwata walibadilishana na Kampuni ya Agritanza Limited baada ya kuona eneo lililobaki halifai kujengwa chuo kikuu kutokana na ufinyu wake.
Alidai kuwa awali eneo hilo lilikuwa kubwa lakini miaka ya 2000 lilianza kumegwa na kuzigawia baadhi ya taasisi na wafanyabiashara na kwamba tume iliundwa na kubaini kwamba hayo yalifanyika kinyume na utaratibu.

“Baada ya kumegwa eneo lililobakia ni finyu ambalo halitoshi kujengwa chuo kikuu. Mimi nilikuwapo wakati Baraza la Wadhamini wa Bakwata wakijadili jinsi ya kupata eneo kubwa na kuijadili Kampuni ya Agritanza iliyokuwa na eneo la ekari 40 Kisarawe ili tubadilishane,” alidai.

Shahidi huyo aliongeza kuwa Agritanza ilikubali kubadilishana maeneo na kwamba wao walichukua ekari nne zilizopo Markaz (Chang’ombe) na Bakwata ikachukua ekari 40 zilizopo Kisarawe.

“Hayo yalifanyika baada ya kupata baraka kutoka katika Baraza la Maulamaa lililokaa na kuamua hivyo Januari 22, 2011,” alisema shahidi huyo na kuongeza:
“Baada ya kufanyika mabadilishano, Agritanza walianza kushughulikia usajili wa kiwanja namba 311/3/4 na walipata. Hivyo kwa sasa ni wamiliki halali, tulishamalizana nao.”

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa eneo hilo Serikali ililitoa kwa Wamisri kwa ajili ya kujenga chuo chini ya usimamizi wa Bakwata.
Alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba huo uliosainiwa mwaka 2003, endapo Wamisri wataondoka Tanzania watarejesha eneo hilo katika umiliki wa Bakwata.
Shahidi huyo pia alitoa kielelezo cha makubaliano ya Baraza la Wadhamini wa Bakwata na Agritanza, kuhusu kubadilishana uwanja.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Juma Nassoro alipinga kwa madai kwamba kisheria walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho mahakamani.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kweka alidai kuwa barua halisi wanayo na kwamba ipo katika kumbukumbu za Bakwata, huku akisisitiza kuwa shahidi anastahili kutoa kielelezo hicho kwa sababu saini yake ipo.

Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo, alikikataa kielelezo hicho akisema Serikali ilitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho.

Hakimu Nongwa alisema kwa kuwa barua halisi ipo wanatakiwa kuiwasilisha mahakamani, lakini akasema endapo barua halisi haipo, basi taarifa ya jana itatambulika kuwa notisi na wataruhusiwa kuiwasilisha.

No comments:

Post a Comment