Monday, November 26, 2012

Kesi ya Kakobe Aprili mwakani

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga kuanza kusikiliza ushahidi wa walalamikaji katika kesi ya ubadhirifu inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa la Full  Gospel Bible Fellowship (FGBC), Zakaria Kakobe Aprili 2, mwakani.
 
Pia, mahakama hiyo imetoa siku 14 kwa pande zote kukubaliana na kuwasilisha mahakamani hoja au mambo yanayobishaniwa, ambayo ndiyo yatakayotolewa ushahidi.
Amri hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Jaji Iman Abood, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo wakati wa mkutano wa makubaliano wa jinsi ya kuendesha kesi hiyo.
Jaji Aboud amepangiwa kusikiliza kesi hiyo baada ya juhudi za usuluhishi zilizofanywa na Jaji Augustine Shangwa kushindikana, kutokana na Askofu Kakobe kukataa usuluhishi huo.
Katika mkutano huo wa makubaliano ya kuendesha kesi hiyo, kila upande ulitaja idadi ya mashahidi wake.
Upande wa walalamikaji unaowakilishwa na Wakili Barnabas Luguwa, ulidai utakuwa na mashahidi watano licha ya walalamikaji wenyewe.
Upande wa utetezi unaowakilishwa na Wakili Miriam Majamba, ulidai utakuwa na mashahidi wanane, zaidi ya mlalamikiwa mwenyewe.
Kesi hiyo namba 79/2011 ilifunguliwa Mei 26, mwaka jana na wachungaji watatu wa kanisa hilo; Deuzidelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma.
Hata hivyo, baadaye Mchungaji Kaduma alilazimika kujitoa kutokana na ushauri wa ndugu na daktari, baada ya kupata ajali na kulazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa.
Baadaye, msimamizi wa kanisa hilo wilayani Liwale, mkoani Lindi, Mchungaji Ignas Innocent naye aliwasilisha maombi kutaka kujiunga katika kesi hiyo.
huku akidai ameamua kupigania haki na kwamba, kuna mambo ambayo anataka kuyaweka wazi.
Wachungaji hao wanamtuhumu Askofu Kakobe licha ya mambo mengine, kwa ubadhirifu wa mali na fedha zaidi ya Sh14bilioni na ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo.
Awali, Askofu Kakobe kupitia kwa wakili wake, Miriam Majamba aliwawekea pingamizi la awali walalamikaji hao  akidai hawana haki ya kumfungulia kesi, lakini juhudi zake ziligonga mwamba baada ya mahakama kulitupilia mbali.
Katika pingamizi lake hilo, licha ya kudai walalamikaji hawana haki ya kisheria kumfungulia kesi, kwamba si wachungaji wa kanisa hilo kwani walishafukuzwa tangu mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment