Friday, November 30, 2012

Dk. Slaa ampa somo Mangula

SIKU chache baada ya Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Philip Mangula, kujibu mapigo ya wapinzani wake akisema wanaombeza wanasahau historia yake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amemtaka aweke mikakati hiyo katika vitendo.
Dk. Slaa alidai kuwa kwa sasa Watanzania wamechoka kusikiliza historia, hivyo kama Mangula ana uthubutu aanze kusafisha chama chake kwa kuwaondoa watuhumiwa magwiji wa ufisadi kabla ya kuhangaika na wale waliotoa rushwa kwenye uchaguzi wao.
Wakati Dk. Slaa akitoa somo hilo kwa Mangula, naye mwanasiasa mkongwe nchini, Thomas Nyimbo, amemvaa kigogo huyo wa CCM akisema kuwa ni kama anashindana na kivuli chake kwa kujidanganya kuwa ataitokomeza rushwa ndani ya chama hicho.
Kauli hizo zinakuja siku chache baada ya Mangula kakaririwa na vyombo vya habari akitamba kuwa wanaombeza kuwa hawezi kuitokomeza rushwa CCM wanasahau rekodi yake akiwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Mangula bila kumung’unya maneno aliwataja wafanyabiashara Yusuf Manji na Thomas Nyimbo kuwa ni miongoni mwa watu aliowafutia ushindi wasigombee ubunge baada ya kubainika kujihusisha na rushwa katika kura za maoni mwaka 2000.
Mwanasiasa huyo pia alikumbushia jinsi chama kilivyofuta matokeo ya baadhi ya washindi katika majibo 32 na kuamuru uchaguzi urudiwe baada ya kubaini uwepo wa mizengwe ya rushwa, hivyo akaahidi kuwa wanaombeza wangoje waone ndani ya miezi sita atakavyochukua hatua.
Hata hivyo, katika mahojiano yake na gazeti hili jana, Dk. Slaa aliendelea kumbeza Mangula akisema kama anajisifu kuwa anaweza kuondoa wala rushwa katika CCM, basi aanze na watuhimiwa sugu walioshindikana kung’oka kwenye falsafa ya kujivua gamba.
Alisisitiza kuwa anamshangaa Mangula kwa kujisifu kwa jambo hilo, na kwamba kama kweli anaweza basi atekeleze sera ya kujivua magamba iliyomshinda mtangulizi wake Pius Msekwa na Wilson Mukama.
Alisema kuwa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho ambao wametajwa hadi na wana-CCM wenyewe bado wapo na wanaendelea vema na kazi za kila siku.
“Hivyo kama Mangula ana ubavu aanze na hawa aache kujisifia historia, mambo anayoyataja kwanza Watanzania wengi hawayajui, wanataka kuona sasa,” alisema.

No comments:

Post a Comment