Thursday, November 22, 2012

Marekani kusomesha bure wanafunzi wa familia maskini

22nd November 2012
Chapa
Serikali ya Marekani kupitia ofisi yake ya ubalozi nchini imeandaa mpango maalumu wa kuwasomesha bure wanafunzi wanaotoka kwenye familia za kipato cha chini.
Taarifa hiyo ilitolewa kwenye mkutano uliokuwa unarushwa moja kwa moja kwa njia ya ‘teleconference’ kutoka maeneo mbalimbali duniani katika ofisi za Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliowahusisha wanafunzi kutoka taasisi za elimu ya juu nchini vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), ulilenga kuhamasisha wanafunzi kutoka familia zenye kipato duni kutoka nchi za Afrika ili waweze kupata ufadhili wa kusomeshwa bure na ubalozi huo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vya Marekani.
Mpango huo unalenga kuwawezesha kielimu wanafunzi wanaochukua shahada za masomo mbalimbali na wanaotoka katika familia zenye kipato duni kutoka katika vyuo vya Afrika.
Wasemaji wakuu kwenye mkutano huo walikuwa ni Naibu Waziri Masuala ya Taaluma katika Idara ya Serikali (Das) inayoshughulikia Mambo ya Elimu na Utamaduni (Eca), Megham Curts.
Baadhi ya washiriki waliipongeza Serikali ya Marekani kwa kuanzisha mpango huo utakaowezesha wanafunzi wengi kusoma nje ya nchi.
“Mpango huu umekuja kwa wakati mwafaka, kwani wanafunzi wengi walikuwa wanashindwa kwenda kusoma nje kwa sababu ya gharama, lakini kupitia mpango huu wengi watakwenda kusoma nje,” alisema Thadeus Ruwai’chi, mwanafunzi wa Aru.
Gideon Abeli, mwanafunzi wa UDSM, alisema mpango huo kuwasaidia wanafunzi kupata elimu zaidi nchini Marekani.
Washiriki hao pia waliuomba Ubalozi huo kuuendeleza mpango huo hadi maeneo ya vijijini.
“Nashauri mpango huo ungefika hadi maeneo ya vijijini kwani huko ndiko kuna wanafunzi wengi wasiojiweza,” alisema Anitha Andax, mwanafunzi wa Aru.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment