Saturday, November 17, 2012

CHADEMA yawaangukia Waislamu,

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Said Issa Mohamed, jana alilazimika kusitisha mkutano wake wa hadhara katika Kata ya Njinjo, Wilaya ya Kilwa baada ya ratiba ya mkutano huo kugongana na ratiba ya mkutano wa kusherehekea mwaka wa Kiislamu kwa wakazi wa kata hiyo.
Issa aliyekuwa afanye mikutano miwili kwa siku hiyo ya jana katika muendelezo wa ujenzi wa chama hicho mikoani badala yake alifanya mkutano mmoja katika eneo la Kilwa Kivinje, ambapo wananchi walimuelezea matatizo mbali mbali yanayowakabili.
Akielezea sababu za kuacha kufanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Njinjo na kupisha shughuli za ibada zifanyike, Issa ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Al rahman ulioko Pemba alisema katika mafundisho ya wanazuoni wanasisitiza kuwa yanapokutana mambo mawili muhimu lile lenye umuhimu mkubwa ndiyo hupewa nafasi zaidi.
“ Najua wakazi wa Kilwa mna kiu ya kusikiliza kutoka kwa viongozi wenu wa kitaifa wa chama ila imani zetu ni muhimu zaidi nasi kama CHADEMA tunaheshimu imani ya kila mmoja, nawaombeni tuvumilie hali hii na kama Mungu akijaalia tunaweza kufanya mkutano wakati mwingine,” alisema Issa.
Kufuatia kauli hiyo wananchi waliokusanyika kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo akiwamo, Sheikh Juma Njumpo walisema wamefurahishwa na hali hiyo ambayo inawaondolea dhana kuwa CHADEMA haiheshimu Uislamu.
Katika mkutano wa pili wa chama hicho uliofanyika katika uwanja wa mkunguni pembezoni mwa Bahari ya Hindi, Issa alisema katika mapambano ya kutafuta uhuru mambo mengi yanaweza yakasemwa kwa wale wanaoonekana kuwa ni tishio kwa utawala ulioko madarakani.
Alisema viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kushirikiana na maafisa wa serikali wameamua kwa makusudi kusambaza uvumi wa kuwa CHADEMA ni ya Wakatoliki pasipo kuangalia athari ya matamshi hayo kwa mustakabali wa taifa la Tanzania.
Aliongeza kuwa watu hao wenye uroho wa madaraka wapo tayari kuona watanzania wanaangamia kwa propaganda za udini na ukabili ili wao waendelee kubaki madarakani huku mikono yao ikiwa inanuka harufu ya damu za waliowaangamiza kwa kauli zao.
Akizungumzia namna walivyoshindwa kushirikiana na Chama cha wananchi (CUF) Issa alisema CHADEMA ilijitahidi zaidi ya mara mbili kuwataka waungane katika maeneo mbali mbali kwa ajili ya kuing’oa CCM ambapo profesa Lipumba aliwakatalia kwa njia ya ujumbe mfupi wa mkononi.
Awali wananchi wa Kilwa Kivinje walimueleza makamu huyo kuwa katika wilaya yao kumekuwa na matatizo mengi ikiwamo miradi kutokuwa na ubora ukosefu wa huduma za msingi na hata kukosekana kwa mabweni ya wanafunzi hali inayowalazimisha wanafunzi hususan wa kike kushindwa kumaliza ngazi mbalimbali za elimu
chanzo-Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment