Friday, November 16, 2012

Mgogoro wa kidini waingia Mashuleni,Sekondari ya kibiti yafungwa

 
SHULE ya Sekondari Kibiti imeifungwa shule kwa madai ya mgogoro wa kidini hivyo wanafunzi kupewa saa mbili kutoonekana shuleni hapo vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Kufungwa kwa shule hiyo kumefikiwa na Bodi iliyokutana  na kuamua kuifunga shule hiyo kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na hisia za kidini zinazozidi kukua kwa kasi shuleni hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu, amethibitisha kufungwa kwa shule hiyo.

“Sipo Rufiji lakini nimejulishwa kuhusiana na kufungwa kwa shule hiyo,”alisema kwa ufupi.

Chanzo cha kufungwa kwa shule hiyo inadaiwa kuwa ni malalamiko ya pande zote mbili baina ya wanafunzi Waislam na Wakikristo ambao wamekuwa wakilaumiana kila upande kudhalilisha dini ya mwenzake hapo shuleni.

Mmoja wa wanafunzi hao wa dini ya kiislam ambaye aliomba asitajwe jina na kudai kuwa waislam wanalalamika kuwa wakiwa wanafanya ibada katika eneo hilo wenzao wa dini ya kikristo huwafanyia fujo.

Alisema kuwa sababu nyingine ni kwamba wanafunzi wenzao siku moja walikwenda kutafuta nyama ya nguruwe na kuja kuitumia katika vyombo vinavyotumika shuleni hapo.

Kwa upande wa wanafunzi wa kikristo wao wanasema kuwa wanafunzi wenzao walichana chana Biblia na kuchoma ofisi yao ya kidini iliyopo hapo  shuleni .

Alisema kuwa bodi ya shule imelazimika kuifunga shule hiyo kwa muda usiojulikana ili kuepuka vurugu kutokea shuleni hapo ili wapate muda wa kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.

Mmoja wa wanafunzi hao alisema kuwa wanafunzi hao walilalamikia suala hilo kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi na ndipo kukawa na mgomo wa hapa na pale wakiutuhumu uongozi wa shule hiyo kwa kushindwa kuthibiti malalamiko hayo.

 Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Mkuu wa shule hiyo, Leslaus Kihongosi alithibitisha kufungwa kwa shule hiyo lakini akasema kuwa hawezi kuwa msemaji wa suala hilo kwa kuwa sio mmiliki wa shule hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji anayedaiwa kuwa mmiliki wa shule hiyo  Nasoro Mwingira alipoulizwa kuhusiana na kufungwa kwa shule hiyo alisema kuwa amepata taarifa za tukio hilo.

“Nasema kwa sasa siwezi kuzungumza jambo lolote kwa kuwa naelekea kwenye tukio  nipo njiani,”alisema.

Diwani wa kata ya Mtawanya iliyopo shule hiyo ya kitaifa,  Rashidi Mkinga alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa analisikia mitaani na hakushirikishwa katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo na yeye hawezi kusema lolote.

Haijafahamika mgogoro wa kidini baina ya wanafunzi wa dini mbili hizo umeanza lini kutokana na wahusika kukwepa kulizungumzia suala hilo huku wakitupiana mpira.
chanzo-Mwananchi

No comments:

Post a Comment