Saturday, November 17, 2012

Simba sc Kwaendelea kuwaka Moto,Rage alisambaratisha Tawi la Mpira Pesa

MWENYEKITI wa Simba, Ismail Rage amelifunga Tawi la wanachama wa timu hiyo linaloitwa Mpira Pesa kwa madai ya kukiuka katiba ya klabu hiyo, pia amevunja kamati zote ndogondogo za timu hiyo.

S
Rage pia amemfuta uanachama mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa, Awadhi Masoud pamoja na Ali Bane kwa madai ya kutoa siri za klabu pamoja na kufanya ubabaishaji kwa kutumia risiti feki na kushindwa kulipa ada ya uanachama kwa miaka miwili mfululizo.

Uamuzi huo wa Rage kulifuta uanachama tawi la Mpira Pesa umekuja siku chache baada ya viongozi wa tawi hilo kuomba wanachama 698 wa Simba kujitokeza kusaini fomu ili kuitisha mkutano wa dharura kwa lengo la kujadili matatizo ya klabu hiyo pamoja na kutokuwa na imani na uongozi wa sasa.

Wanachama hao waliunda kamati ya kukusanya saini hizo wakiongozwa na Bane (Mwenyekiti),  Masoud (Katibu) na wajumbe Hamis Omar, Chuma Suleiman, Said Kubenea, Mkoma Hamis, Sophia Lubuva na Omari Mnkonje.

Rage alisema,"Kuna baadhi ya wanachama siyo waadilifu na wapo kwa ajili ya kuleta migogoro ndani ya klabu yetu. Nilichoamua na kamati yangu ni kufuta Tawi la Mpira Pesa pamoja na watendaji wake."

Alisema,"Kama wanataka kuwa wanachama tena wanapaswa kujiandikisha upya, lengo hasa ni kumaliza tabia za udanganyifu zinazofanywa na watu wachache."

Pia, Rage alisema kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mechi za ligi, kamati yake imeamua kuvunja kamati zote na itaunda upya kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

"Nimeamua kuvunja kamati zote na nitakaa na kuunda upya. Nataka nichague kikosi upya kitakachorudisha hadhi ya Simba. Kwa sasa wanachama wanapaswa kuwa makini na kuisapoti timu yao kwa umoja,"alisema Rage.

Wakati huohuo, habari kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Simba zinadai kuwa kocha Milovan Cirkovic ametupiwa virago rasmi na nafasi yake amepewa Twalib Hilal huku nafasi wa meneja wa timu akipewa Jamhuri Kihwelu 'Julio'.

"Baada ya mkutano wa juzi viongozi walikubaliana kumtimua Milovan na sasa timu itakuwa chini ya Hilal na Kihwelu," kilisema chanzo hicho cha habari.

Katika hatua nyingine, Rage amemwomba radhi nahodha wa Simba, Juma Kaseja kutokana na kitendo cha kudhalilishwa na mashabiki kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar na kumtaka asahau yaliyopita.

Pia Rage alikanusha tuhuma za uongozi wa Azam za kudai wao wanahusika kutoa rushwa kwa wachezaji wa Azam huku akidai wapo tayari kushirikiana nao katika kutafuta ukweli.

Alisema endapo kiongozi yeyote wa Simba atabainika kuhusika na jambo hilo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufutwa uanachama.

No comments:

Post a Comment