Sunday, November 18, 2012

RCO Kilimanjaro atajwa magendo ya sukari

MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi, ameingia katika kashfa akihusishwa na tuhuma za kuwalinda na kuwakumbatia wafanyabiashara wanaojihusisha na usafirishaji wa sukari kwenda Kenya kwa njia za magendo maarufu kama njia za panya.
Tuhuma hizo zimo kwenye taarifa ya siri ya kurasa tano iliyotumwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro hivi karibuni na wananchi wanaojipambanua kama raia wema na wazalendo wanaokerwa na ufisadi na kumtaja RCO huyo kuwa ndiye kikwazo katika mapambano dhidi ya biashara za magendo mpakani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ambayo Tanzania Daima imefanikiwa kuipata nakala yake pia imewataja Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mwanga na Rombo pamoja na Msaidizi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Himo kilichoko wilaya ya Moshi.
Pia wamo maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka ofisi kuu ya mamlaka hiyo na wale walio katika Kituo cha Ushuru na Forodha katika mpaka wa Holili ulioko wilayani Rombo ambao wanatuhumiwa kufumbia macho magari ya sukari yanayopita karibu na kituo hicho.
Hata hivyo, RCO Ng’anzi hakuwa tayari kujibu tuhuma hizo alipoulizwa na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki na kutaka aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, kwa kile alichodai yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi na kwamba hana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari moja kwa moja.
Alipoelezwa kuwa tuhuma hizo zinamhusu yeye binafsi kama RCO na kwamba RPC hawezi kumsemea mtu binafsi, Ng’anzi alisisitiza kuwa yeye si msemaji wa jeshi la polisi na kwamba hana mamlaka ya kuzungumza na moja kwa moja na vyombo vya habari.
“Wasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, yeye ndiye msemaji na sio mimi. Asante sana, mimi si msemaji, sina mamlaka ya kuzungumza moja kwa moja na vyombo vya habari,” ulisomeka ujumbe mfupi kutoka katika simu ya kiganjani ya RCO alioutuma kwa mwandishi wa habari hizi.
Taarifa hiyo imefichua kuwa wafanyabaishara hao wamekuwa na mahusiano ya karibu na RCO huyo na humpigia simu pindi wanapokamatwa na askari wa ngazi ya chini ambapo inadaiwa amekuwa akiwakaripia askari hao na kuwaamuru waondoke mara moja katika maeneo yanakopita magari hayo.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini wastani wa magari makubwa aina ya Fuso 12 hadi 15 yaliyosheheni sukari yamekuwa yakivuka mpaka na kuingia Kenya huku polisi na TRA wakidaiwa kuwa vinara wa kupokea rushwa na kuyaachia magari hayo yapite machoni mwao.
Njia zinazotumiwa na wasafrishaji hao ambao kwa sasa wamejijengea mtandao mkubwa ndani ya TRA na polisi ni kutoka mji wa Himo kupitia Barabara ya Lower Road hadi yalipo machimbo ya mchanga aina ya pozolana na kuingia Kenya sehemu inayojulikana kwa jina la Kwa Mandara ambapo ni mita chache kutoka kituo cha forodha cha Holili.
Njia nyingine ni kutoka katika mji huo wa Himo kupitia Marangu, Mwika, Mamsera, Ibukoni wilayani Rombo na kuingia katika kijiji cha Munga kilichoko mpakani mwa Tanzania na Kenya ambako magari hayo hupata urahisi wa kuingia Kenya eneo linalofahamika na polisi wa Rombo liitwalo Chumvini.
Kwa wilaya ya Mwanga magari yaliyosheheni sukari ya magendo huanzia safari zake katika eneo maarufu la Njiapanda ya Himo baada ya kupakia sukari mjini Moshi na kuelekea vijiji vya Kileo na Mnoa kabla ya kuingia Kenya eneo maarufu la Madarasani au Kitobo ambako hushusha sukari hiyo na kupakiwa kwenya magari ya Kenya.

No comments:

Post a Comment