Sunday, November 18, 2012

Rufaa ya Serikali dhidi ya ACP Zombe kuanza kusikilizwa

JOPO la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani nchini litasikiliza rufaa ya Serikali dhidi ya hukumu iliyompa ushindi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe pamoja na wenzake, Mwananchi limebaini.
 
Zombe na wenzake waliachiwa huru Agosti 17, 2009 na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya ya makosa ya mauaji ya kukusudia yaliyokuwa yakiwakabili.
Watuhumiwa hao wanarejea tena mahakamani, ikiwa imepita miaka 3 na miezi 3 tangu hukumu hiyo ya kuwaachia huru ilipotolewa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu wakati huo, Salum Massati. Hivi sasa Massati ni Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka Mahakama ya Rufaa na kuthibitishwa na baadhi ya maofisa ndani ya mahakama hiyo zinasema rufaa hiyo itaanza kusikilizwa mwezi ujao.
Mwananchi limefanikiwa kuiona ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani ambayo inaonyesha kuwa rufaa dhidi ya Zombe na wenzake itaanza kusikilizwa tarehe 11Desemba mwaka huu saa 3:00 asubuhi na Majaji William Mandia, Nathalia Kimaro na Katherine Oriyo.
Watuhumiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Siku chache baada ya kuachiwa huru, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu, akidai kuwa Jaji Salum Massati aliyesikiliza kesi hiyuo alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao.
Katika hukumu yake, Jaji Massati alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hapo bila kuacha mashaka.
Pia Jaji Massati alisema kuwa amebaini kuwa wauaji halisi hawajafikishwa mahakamani na kwamba kutokana na kutokuwepo kwao mahakami, mashtaka dhidi ya washtakwa waliokuwapo mahakamani hayawezi kutengenezeka, hivyo akaiagiza Jamhuri kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wauaji halisi.
Hoja za DPP
DPP katika rufaa yake namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009, amebainisha sababu 11 ambazo zimemfanya apinge hukumu hiyo, akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.
Katika hoja hizo, DPP amedokeza kile anachokiita upungufu katika hukumu hiyo, kwa kila mshtakiwa.
DPP anadai kuwa jaji Massati alipotoka, alishindwa kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu mashtaka ya jinai na kwamba alijichanganya sana katika hukumu hiyo.
Anadai na kueleza kushangaa Jaji kushindwa kuwatia hatia washtakiwa wote licha ya kwamba kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira wa kutosha kuwatia hatiani.

No comments:

Post a Comment