Friday, November 23, 2012

VIONGOZI SADC KUKUTANA,NI JUU YA USALAMA WA DRC.


Membe alisema leo na kesho, viongozi wakuu wa Sadc watakutana jijini Kampala, Uganda kujadili namna ya kuinusuru DRC hata kama UN itaendelea kushikilia msimamo wake, viongozi hao watatoa uamuzi mgumu.
Kuhusu tuhuma kwamba Serikali ya Rwanda pamoja na Uganda zinawasaidia waasi, Membe alisema inasikitisha viongozi wa nchi hizo kutokaa na kumaliza tofauti zao na katika mkutano wa leo na kesho, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda, watahudhuria.
Waasi wa M23 waliibuka Aprili mwaka huu kwa madai ya kupinga maazimio ya Machi 23 mwaka 2009, yaliyofikiwa wakati Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, walipokuwa wakisuluhisha mgogoro wa DRC.
Vitendo vya wapiganaji hao wa M 23 vimezua wasi wasi wa kuzuka upya kwa mapigano nchini DRC, ambako takriban watu milioni tano waliauawa kufuatia mapigano yaliyoanza mwaka wa 1997 na kumalizika mwaka 2003.
Jumanne wiki hii, waasi hao waliuteka Goma uliopo Mashariki mwa DRC unaoelezwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini.
Hii ni mara ya kwanza kwa waasi kufanikiwa kuteka Goma tangu kumalizika kwa mapigano mwaka wa 2003.
Kumekuwa na taarifa za Serikali ya Rwanda kuhusika kuwasaidia waasi hao, lakini imekuwa ikikanusha.
Baraza la Usalama la UN limelaani kutekwa kwa mji huo na mapigano yameelezwa kuwa mabaya zaidi tangu waasi walipoanzisha vita Julai mwaka huu.
Tayari Rais wa DRC, Joseph Kabila, ambaye aliapa kuulinda Goma, amekubali kuanzisha mazungumzo na waasi hao. Juzi wapiganaji hao wa M23 waliuteka mji wa Sake, ulioko takriban kilomita 27, kutoka Goma.
Ripoti zinasema wapiganaji hao sasa wanajiandaa kuelekea eneo la Kusini hadi Bukavu, takriban kilomita 230 kutoka Goma.
Wakati huo huo; Membe amesema taarifa ya kikao cha kamati ya mambo ya nje kuhusu suala la Malawi imekabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na kwamba lengo ni kwa Rais Kikwete kukutana na Rais wa Malawi, Joyce Banda, ili kutafuta mwafaka.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment