Friday, November 16, 2012

Kikosi 2015 cha ccm

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeunda Sekretarieti mpya katika uongozi wake, huku wakongwe wakirejeshwa, akiwamo Abdulrahaman Kinana aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Kinana mwanasiasa wa siku nyingi ambaye amekitumikia chama hicho kwa miaka 25, anachukua nafasi ya mtangulizi wake, Wilson Mukama ambaye ameng’olewa katika nafasi hiyo na kuweka rekodi ya kuwa Katibu Mkuu aliyekaa kwa muda mfupi wa miaka miwili tu.

Wengine katika Sekretarieti iliyotangazwa jana na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa, Zakhia Meghji, Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatibu na Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha- Rose Migiro.

Akitangaza safu hiyo mpya ya uongozi baada ya kumalizika kikao cha  Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa White House jana, Rais Kikwete aliwataja wengine aliowateua kuwa ni Vuai Ali Vuai ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Alisema Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amepandishwa kutoka Katibu Uchumi na Fedha na kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati.

Alisema Meghji  atakuwa Katibu wa Uchumi na Fedha akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Nchemba, wakati Khatib ameteuliwa kuwa katibu wa Oganaizesheni ya chama hicho, nafasi ambayo katika Sekretarieti iliyopita ilikuwa ikishikiliwa na Asha Abdallah Juma.

Dk Migiro ameteuliwa kuwa Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Kwa mujibu wa kanuni za CCM, mawaziri hawaruhusiwi kuwa watendaji katika sekretarieti ya chama, hivyo Makamba asingeweza kuteuliwa tena isipokuwa kwa sababu maalumu.

Dk Migiro kama ilivyo kwa Meghji aliwahi kushika wadhifa huo kabla ya kuteuliwa kwenda Umoja wa Mataifa. Rais Kikwete alisema chama hicho kimemteua Nape Nnauye kuendelea na wadhifa wake wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama.

Alisema ameshindwa kuteua wajumbe wa Kamati Kuu kwa sababu wajumbe wa Nec bado ni wapya na kwamba apewe muda wa kuangalia atakaowateua.

“Uteuzi wa Kamati Kuu, utafanyika baadaye kwa sababu Nec hii ina watu wazuri na wapya, hivyo nipeni muda niangalie nani nimteue kuingia katika Kamati Kuu,” alisema.

Walioachwa

Mukama aliyechukua nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM 2010, amepewa jukumu la kusimamia uanzishwaji wa chuo cha chama hicho.

Katika uongozi wake, kiongozi huyo amekuwa akilalamikiwa na makada wa CCM ambao wamekuwa hawaridhishwi na utendaji wake tangu alipoteuliwa, hasa kuhusu utekelezaji wa mpango wa kujivua gamba ambao ulilenga kuwang’oa watuhumiwa wa ufisadi.

Alitikiswa na siasa za makundi ambayo yamekuwa yakipata nguvu kila kukicha, kutokana na kujipanga kuwania urais wa 2015 kupitia CCM, na katika Uchaguzi Mkuu wa chama hicho, alionekana kushindwa kukimudu chama kutokana na kushamiri kwa rushwa.

Mukama akizungumzia uteuzi wa kuongoza uanzishwaji wa chuo cha CCM alisema amefurahi kufanya kazi hiyo.

Alisema: “Nimefurahi sana, sina wasiwasi na majukumu mapya ambayo nimepewa, nitayamudu.”


Chiligati kwa upande wake anaondoka katika chama hicho baada ya kudumu kwa muda mrefu akiwa mjumbe wa Sekretarieti.

Awali alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi na baadaye alipandishwa wadhifa na kuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), nafasi iliyompa misukosuko hasa katika kipindi ambacho CCM kilijaribu kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Kwa upande wake, Asha Abdallah Juma, yeye ameachwa kutokana na umri, hali ambayo imekuwa ikimfanya ashindwe kushiriki kikamilifu katika harakati za kisiasa ndani ya CCM.

Kada huyo wakati wa uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki mwezi Aprili mwaka huu, alikuwa akitembelea fimbo na hakuwa na uwezo wa kusimama jukwaani kwa muda mrefu.

Kikosi cha 2015

Makada wapya walioteuliwa wanaungana na mkongwe mwingine, Makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula aliyerejeshwa katika uongozi wa juu wa chama, baada ya kuwa nje kwa miaka mingi.

Mangula aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati wa uongozi wa Benjamin Mkapa alipata nafasi hiyo baada ya kukosa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Iringa katika uchaguzi uliopita. Baada ya kukosa nafasi hiyo aliendelea na shughuli za kilimo mkoani humo.

Mangula kama alivyo Kinana wanatajwa kuwa watu makini na kuwepo kwao katika nafasi za juu za uongozi wa CCM ni ishara kwamba huenda chama hicho kimeamua kujipanga ipasavyo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Mangula ni mmoja wa makada wa CCM walioitwa kuokoa jahazi la chama hicho lisizame katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga, ambako anatajwa kuwa alisaidia kuwabaini hata makada ambao walikuwa wakitoa taarifa za uongo kuhusu uchaguzi huo.

Kinana kama alivyo Mangula, amejizolea sifa ya kuwa kiongozi mkuu wa kampeni za CCM tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi nchini 1995, na tangu wakati huo chama hicho hakijawahi kushindwa.

Siku chache zilizopita alitangaza rasmi kustaafu siasa ndani ya CCM, hatua ambayo iliwashtua sana makada wa chama hicho wakiwamo vigogo ambao tayari walikuwa wameanza kumshawishi kukubali uteuzi wa nafasi ya Katibu Mkuu.

Habari kutoka ndani ya CCM zinasema, kulikuwa na kazi kubwa ya kumshawishi kukubali wadhifa huo na kwamba alitoa masharti magumu ambayo vigogo wa chama hicho walilazimika kuyakubali ili “kukinusuru chama”.

Kauli za wateule

Akizungumzia kuteuliwa kwake, Kinana alisema ameupokea kwa furaha uteuzi huo ingawa ni dhamana nzito kuibeba.

Hata hivyo, alisema atajitahidi kadiri ya uwezo wake kumsaidia Mwenyekiti wa chama hicho kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM.

Kinana alisema ingawa hivi karibuni alitangaza kustaafu uongozi ndani ya chama hicho, lakini aliombwa na Rais Kikwete amsaidie, hivyo asingeweza kukataa.

Alisema uamuzi wa kustaafu uongozi ulikuwa uamuzi wake binafsi baada ya kukaa katika uongozi wa chama kwa miaka 25.

Kinana alisema aliona ni vyema kukaa pembeni ili watu wengine ndani ya chama hivyo hususan vijana kuchukua nafasi za uongozi.

Kuhusu uadilifu ndani ya chama hicho, alisema atatekeleza uamuzi wote wa vikao na kwamba watautengenezea programu ya utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Meghji alisema amefurahi kuteuliwa katika nafasi hiyo ambayo inamwezesha kukitumikia chama tena.

Alisema nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama ina changamoto nyingi hasa kwa wakati huu ambapo chama hicho, kimeamua kujitegemea kiuchumi.

Hata hivyo, alisema anaamini kuwa atashirikiana na viongozi na wanachama wengine ili kufanikiwa kwa mipango hiyo ya chama.

“Naamini kuwa tutafanikiwa kufikia lengo hilo la chama kwa sababu tutashirikiana wote,” alisema.

Naye Dk Migiro alisema ameupokea uteuzi huo kwa furaha, kwa sababu ni kazi ya kukijenga chama chao.

Alisema kwake yeye ni heshima kubwa kupewa majukumu hayo ya kuitumikia nchi yake kupitia CCM.

“Ni heshima kubwa kupewa majukumu haya ya kuitumikia nchi yangu,” alisema.

Naye Mwingulu alisema ameufurahia uteuzi huo kwa sababu hakutarajia kuwa katika timu hiyo mpya.

Alisema  amefurahishwa kupangwa katika timu mpya ya uongozi wa chama hicho ambayo anaamini ni ya ushindi.

“Nimepokea uteuzi, kwa mshtuko mkubwa na furaha , nimefurahishwa na timu mpya ambayo nimo ndani yake,” alisema.

No comments:

Post a Comment