Wednesday, November 28, 2012

Safari ya mwisho ya Sharo Milionea

MAELFU ya waombolezaji jana walijitokeza kushiriki mazishi ya msanii Hussein Ramadhan maarufu kwa jina la Sharo Milionea, huku mamia wakizirai baada ya kushindwa kujizuia wakati mwili wake unawekwa kaburini.
Maelfu ya waombolezaji jana walijitokeza kushiriki mazishi ya msanii Hussein Ramadhan maarufu kwa jina la Sharo Milionea, huku mamia wakizirai baada ya kushindwa kujizuia wakati mwili wake unawekwa kaburini. 

Mwili wa msanii huyo ulizikwa jana kijijini kwake Lusanga wilayani Muheza saa 7 mchana, katika tukio lililomshirikisha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.

Waombolezaji walianza kumiminika kijijini Lusanga tangu juzi jioni na idadi yao iliongezeka zaidi jana asubuhi. Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi.Sala ya mazishi iliongozwa na Sheikh Twaha Juma ambaye baadaye aliamuru jeneza hilo kupelekwa makaburini, ambako waombolezaji kadhaa walipoteza fahamu.

20 wapelekwa hospitali
Miongoni mwa matukio yaliyojitokeza katika msiba huo ni baadhi ya waombolezaji kupoteza fahamu msibani.Matukio tofauti ya watu kuzirai yalitokea wakati mwili wa msanii huyo ulipokuwa unapelekwa nyumbani kwao kijijini Lusanga ukitokea Hospitali Teule ya Wilaya ambako ulihifadhiwa tangu alipopata ajali Jumatatu usiku na wakati wa mazishi.

Miongoni mwa waliopoteza fahamu katika msiba huo ni wasanii na waigizaji wa filamu waliokuwa wakiigiza na Sharo Milionea wakati akiwa katika kundi la AL Riyam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MC wa shughuli hiyo, Steve Nyerere, zaidi ya watu 20 walipoteza fahamu katika msiba huo na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Muheza.

DC Mgalu aliwaomba waombolezaji kutokuwa na shaka juu ya waliopoteza fahamu kwa kuwa madaktari maalumu walikuwa wameandaliwa hospitalini hapo kwa ajili ya kuwapa huduma.
Mwananchi lilifika katika hospitali Teule na kukuta waliokuwa wamepoteza fahamu, wengi wao wakiwa ni wasichana, wakipata huduma huku wengine wakiomba kupewa ruhusa ili wakahudhurie maziko.

JK atuma rambirambi
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kutokana na vifo vya wasanii watatu vilivyotokea hivi karibuni, kikiwamo cha Sharo Milionea.

Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete ameshtushwa na vifo hivyo vya ghafla.
Wasanii hao ambao walifariki dunia katika mazingira tofauti ni Mwigizaji wa Kundi la Kaole, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ aliyefariki dunia hivi karibuni kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.

Msanii mwingine ni mwigizaji wa filamu, John Maganga aliyefariki Novemba 24, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno kutokana na taarifa za vifo vya wasanii hawa ambao kwa hakika mchango wao mkubwa katika tasnia ya muziki na maigizo hapa nchini ulikuwa unatambuliwa na kuthaminiwa na wananchi wengi,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.

Vile vile, mke wa Rais Kikwete, Mama Salma alituma salamu za rambirambi zilizosomwa na DC Mgalu, kuwa ameguswa na msiba huo na kuwataka ndugu wa marehemu na wasanii wengine kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.
Kwa mujibu wa Mgalu, Mama Salma alituma salamu hizo akiwa Mwenyekiti wa Mfuko wa Wanawake na Maendeleo (WAMA).

“Mke wa Rais kama mnavyojua ni mama wa Watanzania wote na ni mama wa wasanii, hivyo msiba huu wa Sharo Milionea umemgusa sana na ameitaka familia ya marehemu kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha majonzi,” alisema Mgalu.

Wenye sare za CCM
wazomewa
Katika msiba huo watu waliokuwa wamevalia sare za CCM walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na waombolezaji ambao walisema hakukuwa na haja ya kujitambulisha kiitikadi katika msiba huo.

Kundi la vijana waliokuwa kando ya barabara ielekeayo kitongoji cha Jibandeni, nyumbani kwa mama mzazi wa marehemu, waliwazomea watu hao huku wakisema kuwa huo haukuwa msiba wa CCM bali ni wa wasanii wa filamu.

Vijana hao walieleza kushangazwa kwao na kitendo cha makada hao kuvaa sare katika msiba huo wakati kiongozi wao ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwasili msibani hapo akiwa amevaa nguo za kawaida.

No comments:

Post a Comment