Friday, November 23, 2012

Tutapeleka jeshi Kongo - Membe,pia awatupia lawama walinda amani wa UN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Serikali ya Tanzania imesema iko tayari kupeleka majeshi yake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kukabiliana na waasi wa kundi la M23 ambao wanapingana na serikali ya nchi hiyo na kuuteka mji wa Goma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema Tanzania imelaani waasi kuteka mji wa Goma na kwamba ni jambo lisilokubalika wala kuvumilika tena.
Membe alisema kitendo cha waasi kuuteka mji huo na kutangaza kutaka kuteka miji zaidi ukiwamo wa Bukavu ni jambo la hatari na linalopaswa kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
Alisema msimamo wa Tanzania upo bayana kwamba iko tayari kupeleka kikosi kimoja cha wanajeshi 800 na nchi nyingine za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) zitachangia majeshi mengine ili kufikia wanajeshi 4,000 wanaohitajika.
Hata hivyo, Membe alisema majeshi ya Tanzania yataondoka nchini baada ya nchi nyingine kukubali kutoa idadi nyingine ya wanajeshi wanaohitajika na pia kuafikiana namna ya kuvamia nchi hiyo kukabiliana na waasi.
Alisema nchi za Sadc zipo tayari kupeleka majeshi ya kuisaidia serikali ya DRC, lakini katika hali ya kushangaza Umoja wa Mataifa (UN), umezizuia huku ukitazama waasi wakiteka miji na kufanya uhalifu wa kibinadamu.
Waziri huyo alisema hali ya DRC inasikitisha na inatisha, lakini UN imezuia wanajeshi kupelekwa nchini humo kwa kisingizio kwamba kuna majeshi yanayolinda amani uko wakati hayana nguvu kisheria za kupambana na waasi wala kupigana vita.
“Tunasikitishwa na wenzetu wa vikosi vya UN kuendelea kuangalia tu hali ya usalama, lakini havina uwezo wa kukabiliana na vita. Tulilalamika kwamba ingawa kuna majeshi ya UN, lakini hayana uwezo wa kukabiliana na wapinzani. Wanachofanya ni kuangalia tu wapinzani wako wangapi, wako wapi, wakimbizi wangapi wamepatikana na wangapi hawana chakula, tunasema kwa utaratibu huu hatufiki mbali,” alisema Membe.
Alisema dawa pekee ya kuinusuru DRC ni kwa Sadc kupeleka jeshi nchini humo kwa ajili ya kulinda mipaka na kuwalazimisha waasi waweke silaha chini ili utawala wa sheria uwepo nchini au majeshi ya UN yaliyopo nchini humo kuruhusiwa kupambana na waasi hao.
“Tanzania imekubali kujitolea kupeleka kikosi kimoja Kongo na hata nchi nyingine za Sadc ziko tayari kufanya hivyo hata kesho (leo) asubuhi,” alisema Membe.
Alisema kitendo cha waasi wakundi la M23 kuteka Goma kimesababisha wananchi wengi kukimbia makazi yao na wanawake kubakwa na kutangaza kutaka kuuteka miji ya Bukavu na Kinshasa.
Alisema waasi kuachiwa kuteka miji hususani wa Bukavu, Tanzania itaathiriwa vibaya na uhalifu huo kwa kuwa wakimbizi watakimbilia nchini.
“Tumeomba na tunaendelea kuomba kwamba Katibu Mkuu wa UN akipe nguvu kikosi chake kilichopo Goma na Kivu kibali cha kukabiliana na waasi badala ya kuendelea kuangalia amani ikivurugika DRC, kwamba UN wasikubali tena kuona watu wakidhalilika katika nchi yao huku majeshi ya UN yakiangalia tu. Lakini tumeomba pia sisi turuhusiwe kupeleka majeshi yetu yakapambane na waasi,” alisema Membe.
 CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment