Friday, November 16, 2012

Mbunge Mdee awapa matumaini wakazi Babati

MBUNGE wa wa Jimbo la Kawe(Chadema), Halima Mdee,amewataka wakazi wa mkoa wa Manyara kujiandaa kutwaa ardhi na mashamba ya wawekezaji ambayo hayajaendelezwa  kuanzia mwakani.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa michezo Babati, Mdee alisema haiwezekani ardhi yote yenye rutuba nchini kumilikishwa wageni wakati Watanzania wakitaabika.

Mdee ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema wawekezaji hao wamemilikishwa ardhi yenye rutuba kwa kulipa Sh 2000 tu kwa heka kwa mwaka, wakati wao wanatumia mashamba hayo hayo kuwakodishia Watanzania kwa Sh 100,000 kwa mwaka kwa heka.

"Kama mlivyosikia bunge lililopita tumewasha moto bungeni juu ya ardhi na wabunge wa CCM wametuunga mkono, sasa tunasubiri bunge la mwezi wa nne, mwakani kisipoeleweka kaeni mkao wa kula kutwaa mashamba"alisema Mdee.


Alisema tayari pia Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alitoa kauli bungeni ya wawekezaji kupewa mwaka mmoja kuendeleza mashamba la sivyo watapokonywa.


Mdee alisema Watanzania hawawezi kugeuzwa watumwa kwenye ardhi yao na sasa wamechoka ndio sababu Chadema, inataka taarifa ya bungeni juu ya ardhi yote iliyopo nchini, iliyotolewa kwa wawekezaji na iliyobaki.

"Hapa Babati kuna ardhi zaidi ya hekari 250,000 inamilikiwa na wawekezaji Wazungu na Wahindi ambao hawaitumii ardhi yote badala yake wanakodisha kwa Watanzania"alisema Mdee.

Akizungumzia Halmashauri ya Babati, alieleza kusikitishwa na wakazi wa Babati kuwachagua madiwani wote wa CCM na mbunge wa CCM, ambao wameshindwa kuwatetea.

"Mbunge wenu kila siku yupo jimboni kwangu Mbezi Jijini Dar es Salaam, kwani ndiko anaishi muda mrefu, mlimuaacha Paulina Gekur sasa mnajuta"alisema Mdee.

Hata hivyo, alisema yaliyopita si ndwele wagange yajayo katika kuhakikisha wanachagua madiwani na wagombea wa Chadema katika chaguzi zijazo.

Awali Wabunge wa Viti Maalum , Paulina Gekur Rose Kamili na Cesilia Pareso, waliwataka wakazi wa Jimbo la Babati, kubadilika sasa na kutambua kuwa ukombozi wao upo Chadema.

Gekur alieleza kazi aliyofanya katika Halmashauri ya Babati, ikiwepo kuzuia ushuru holela wa machinjio, kuzuia wamachinga kuhamishwa bila utaratibu na kufichua ufisadi katika halmashauri.

"Ndugu zangu japo kuwa mimi nipo mmoja tu katika baraza la madiwani nadhani mnajua kazi kubwa ambayo nafanya kuwatetea"alisema Gekur.

Nao Pareso na Kamili  walisema viongozi wa CCM wameshindwa kuwadhibiti watendaji wa serikali wasiwahujumu wananchi na suluhu ya maisha bora kwa wananchi ni kuchaguwa   Chadema katika nafasi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment