Thursday, November 22, 2012

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amepinga kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amepinga kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika kuwa Serikali ya Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze kusaidia uchunguzi.
Zitto ambaye hivi karibuni aliwasilisha bungeni hoja binafsi ya kulitaka Bunge liazimie kuunda kamati teule ya kuchunguza vigogo hao wanaotuhumiwa, alisema kauli ya Mkuchika ni wazi serikali inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio la Bunge. Katika taarifa yake aliyoiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter jana, Zitto aliwaonya Watanzania wasikubali propaganda hiyo ya serikali.
“Nimeona ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi sawa juu ya azimio la Bunge na kwamba serikali inapaswa kutekeleza azimio na sio kutoa kauli tata za kukata tamaa,” alisema.
Alisema kuwa suala la Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akichangia hoja yake binafsi aliyowasilisha bungeni na pia wakati akileta maombi yake ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge.
“Kama sio sababu mpya ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi serikali inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio la Bunge. Watanzania wasikubali propaganda hii ya serikali,” alisema Zitto.
Alifafanua kuwa, Bunge limeagiza serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa. Akahoji ni kwanini serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi hiyo?
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alihoji kuwa serikali inajaribu kuficha nini na kwanini baada ya wiki iliyopita Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye mabenki ya biashara jijini Dar es Salaam wa namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje halafu leo serikali inakuja na kauli za kukakata tamaa.
“Watanzania wajue kwamba taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao na kuzificha huko,” aliongeza.
Alifafanua kuwa Serikali ya Uswisi hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hili. Ndiyo maana azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya Uswisi.
“Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara baada ya Rais Mobutu Seseseko kuangushwa na Rais Laurent Kabila kule Kongo – Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu,” alisema.
Kwamba Waswisi walitaka Kabila awahakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani, Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha.
Alisema kuwa majibu ya aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo kila nchi inapewa.
“Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivi hivi. Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi.
“Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila aibu mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta,” alisema.
Zitto alionya kuwa hatupaswi kuwa taifa la mazezeta kwani mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa kuimba. Kwamba sasa Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Uswisi badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa bungeni.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), aliitaka serikali ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge.
“Suala hilo sio la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni suala la wananchi. Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya kutekeleza azimio lao,” alionya.
Alisisitiza kuwa, kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliosababisha Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya Tanzania.
“Hatutakaa kimya mpaka tuone mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni salamu tosha kwa mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha na Tanzania sio taifa la kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda atupishe mapema,” alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment