Friday, November 23, 2012

Tamthilia ya EPA inaendelea Maranda, Farijala wahukumiwa tena

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemhukumu kwenda jela miaka miwili kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda, na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kughushi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 3.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (EPA) .
Mbali na hukumu hiyo, Maranda jana aligeuka mbogo kabla ya jopo la majaji kuingia ndani ya ukumbi kutoa hukumu dhidi yake, kwa kuwatolea lugha za vitisho wapiga picha wa magazeti mbalimbali waliokuwa wakitaka kumpiga picha akiwa amekaa ndani ya chumba cha mahakama.
Aliwaambia wapiga picha hao kuwa wamemchosha na kwamba hataki kupigwa picha na endapo mtu angefanya hivyo basi angemfunza adabu kwa kuwa haogopi tena kesi, kwa kuwa kukaa jela Mungu amemuandikia.
Maranda akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi na magereza, alinyanyuka kwenye kiti na kuwafuata wapiga picha na kuanza kukagua kamera ya mpiga picha mmoja kama alikuwa amempiga picha na wakati akifanya hayo, wana usalama hao walikuwa wakimwangalia hali iliyosababisha wapiga picha hao kuingiwa na woga.
Hukumu hiyo ilianza kusomwa saa 8 hadi saa 11:56 jioni na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mugeta, kwa niaba ya wanajopo wenzie, Jaji Samuel Karua na Beatrice Mutungi, ambao walisema washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na makosa sita.
Makosa hayo ni kula njama kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kughushi jina la biashara la kampuni feki ya Lakshmil Textile Mills Co Ltd ya India na hati ya kuhamisha deni iliyoonyesha kampuni ya Maranda na Farijala ya Mibare Farm imepewa idhini ya kudai deni la kampuni hiyo ya India katika BoT.
Mengine ni kuwasilisha nyaraka zilizogushiwa katika Benki ya Afrika na Benki Kuu ambazo zilionyesha nyaraka hizo zilikuwa zimetolewa na Brela, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kujipatia ingizo toka BoT na kuisababishia hasara ya sh bilioni 3.8 ambapo kosa hilo la sita lilikuwa likiwakabili maofisa wa BoT ambao ni mshtakiwa wa 4, 5 na 6 ambao ni (Iman Mwakosya, Ester Komu na Kaimu Katibu BoT, Sophia Lalika ambao walikuwa wakitetewa na Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Ademba Agomba.
Hakimu Mugeta akiisoma hukumu hiyo alisema mahakama imefikia uamuzi wa kulifuta kosa la tano ambalo ni la kujipatia ingizo ambalo linamkabili mshtakiwa 1, 2, 3 ambao ni Farijala Hussein, Rajabu Maranda na Ajay Somai kwa sababu upande wa Jamhuri umefanya makosa ya kujumuisha kiwango cha fedha wanachotuhumiwa kujipatia.
Kwamba mahakama imelifuta kosa hilo na pia imewaachilia huru washtakiwa wote katika kosa la kwanza la kula njama kwa sababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kosa hilo.
Hakimu Mugeta alisema hata hivyo upande wa jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Oswald Tibabyekomya, Shadrack Kimaro, Tumaini Kweka, umeweza kuthibitisha shtaka la kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa na kuisababishia serikali hasara.
Alisema kuwa mashahidi wote saba na vielelezo vya upande wa jamhuri vimeweza kuishawishi mahakama hiyo kuwatia hatiani kwa makosa hayo yaliyothibitishwa na upande wa jamhuri.
Aliongeza kuwa katika kosa la pili, mahakama hiyo imemtia hatiani Farijala peke yake na kwamba atatumikia adhabu kifungo miaka mitatu jela, kosa la tatu ni la Maranda na Farijala ambao wametiwa hatiani na watatumikia adhabu ya miaka miwili jela na kosa la nne mahakama imemtia hatiani Farijala, Maranda na Ajay Somai ambao watakwenda jela miaka miwili.
Kosa la sita ni la kusababisha hasara ambapo mahakama imewatia hatiani maofisa hao wa BoT, Mwakosya, Komu na Lalika ambapo watalipa fidia ya sh milioni 5 kila mmoja na endapo watashindwa watakwenda jela miaka mitatu.
Aidha Hakimu Mugeta alisema mahakama yake imesikiliza ombi la wakili mwandamizi wa serikali, Kimaro, ambaye alitaka mahakama hiyo iwaamuru washtakiwa warejeshe serikalini kiasi cha fedha ambacho serikali imepata hasara lakini imekubaliana na hoja ya wakili wa utetezi Majura Magafu.
Katika hoja yake wakili Magafu alidai kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha maofisa wa BoT walinufaika na kiasi hicho cha fedha ila kuna ushahidi unaonyesha Maranda, Farijala na Somai walinufaika na kiasi hicho cha fedha.
“Kwa sababu hiyo mahakama hiyo inamwamuru Farijala kuilipa serikali fidia ya sh 82,956,400, Maranda sh 616,443,600.10 na Somai sh milioni 400 na endapo watashindwa kuilipa serikali fidia hiyo basi mali zao zitakamatwa. Washtakiwa wangelianza kuitumikia adhabu hiyo kuanzia jana,” alisema Mugeta.
Hii ni kesi ya tatu kati ya 11 za wizi wa fedha za EPA zilizofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Novemba 2008, zilizokwishatolewa hukumu dhidi ya washtakiwa mbalimbali.
Hukumu ya kwanza ni kesi ya jinai Na.1161/2008 iliyokuwa ikimkabili Maranda na Farijala ya wizi wa sh bilioni 1.8 ambapo ilitolewa hukumu Mei mwaka jana, ambapo walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela na kesi nyingine ya EPA ni jinai Na. 1163/2008 ambapo Maranda na Farijala Mei, mwaka huu, walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kwenda jela miaka mitatu.
Hukumu nyingine ni kesi hii Na.1164/2008 ambayo ilitolewa uamuzi jana na washtakiwa wakapatikana na hatia.
Kwa hiyo hivi sasa Maranda atabakia akikabiliwa na kesi nyingine mbili za EPA na Farijala atabakiwa na kesi moja ya EPA ambayo bado haijatolewa hukumu.
Baada ya Hakimu Mugeta kumaliza kutoa hukumu hiyo saa 11:56 jioni, Mwakosya, Komu na Lalika walishindwa kulipa kiasi cha fidia walichoamriwa na mahakama hivyo na hivyo wakaungana na Maranda na Farijala kwenda gerezani.

No comments:

Post a Comment