Saturday, November 17, 2012

Dewji kuwabeba wakulima wa Singida India

MBUNGE wa Singida Mjini, Mohamed Dewji (CCM), amebuni mradi wa kuwainua wakulima kiuchumi kwa kuwawezesha kulima mazao mbadala ambayo yatauzwa nchini India na kwingineko.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dewji alisema mradi huo utawahusisha wakulima 5,000 ambao watapatiwa mbegu na plau.
Aliyataja mazao ambayo yanalimwa kupitia mradi huo kuwa ni choroko, mbaazi na dengu na kwamba amekwisha kuyatafutia soko nchini India ambako kuna soko kubwa.
Alisema wakulima hao wamegawanywa katika makundi ya watu kumi, ambapo kila kundi lina kiongozi mmoja ambaye amepatiwa plau.
“Kuna vikundi 500 na kila kikundi tumekipatia plau moja yenye thamani ya sh 100,000 na jumla ya plau zote ni sh milioni 50,” alisema Dewji.
Pamoja na hilo, alisema ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa wakulima hao wanapatiwa mafunzo lakini pia ameajiri wataalamu wa kilimo ambao wanawafuatilia kila hatua.
Katika hilo, Dewji alisema mazao hayo yatawakomboa watu wa Singida kwa kuwaongezea kipato, tofauti na kile kinachotokana na mazao mengine kama mahindi.
Alisema wanatarajia watakapouza mazao hayo jumla ya sh bilioni mbili zitapatikana na kila mkulima atapata sh 400,000 badala ya sh 160,000 alizokuwa akipata kutokana na kulima mahindi.

No comments:

Post a Comment