Thursday, November 22, 2012

Waliokuwa madiwani CHADEMA wahukumiwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imewaamuru waliokuwa madiwani watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Arusha, kulipa gharama zilizotumika kuendesha shauri lao lililotupwa na mahakama ya mkoa kiasi cha sh milioni 15.1 kwa awamu mbili vinginevyo watapelekwa jela.
Aidha, kila mdaiwa aliamriwa kulipa sh milioni 3.2 ambapo awamu ya kwanza ya sh milioni 1.51 walitakiwa kutoa mara baada ya uamuzi huo kutolewa na kiasi kilichobaki wanatakiwa wawe wamelipa ndani ya kipindi cha miezi miwili toka jana.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Charles Magesa, mbele ya wakili wa CHADEMA, Method Kimomogoro ambaye pia alimtetea Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe katika kesi ya awali ya madiwani hao kupinga kuvuliwa uanachama.
Wajibu maombi katika shauri hilo waliokuwapo mahakamani hapo wakati uamuzi huo ukitolewa ni Reuben Ngowi, Charles Mpanda na Rehema Mohamed, huku wenzao, Estomii Mallah alitoa udhuru wa kufiwa na mwanaye na John Bayo haikufahamika sababu za kutohudhuria.
Hakimu Magesa alisema kuwa, alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ambapo alikubaliana na hoja za wakili Kimomogoro aliyeieleza mahakama hiyo kuwa, wajibu maombi hao hawajaieleza mahakama hiyo kama wana mali zinazoweza kukamatwa endapo watashindwa kulipa deni hilo.
Alisema kuwa, alikubaliana na hoja za wakili huyo wa CHADEMA kuwa wadaiwa hao hawajaionyesha mahakama kama hawana uwezo wa kulipa kwani walikuwa wakiweka na kulipa wakili wa kutetea kwenye mashauri yote waliyokuwa wakifungua sanjari na kulipia gharama mbalimbali za kesi.
Hakimu Magesa alisema kuwa wajibu maombi kupitia wakili Lawena aliyekuwa akiwatetea kabla ya kujitoa, waliridhia kutoa viwango tofauti vya fedha ambapo Mallah ni sh 20,000, Bayo sh 20,000, Mpanda sh 15,000, Rehema sh 15,000 na Ngowi sh 25,000 ambaye tayari ameshalipa sh milioni moja.
Kwamba viwango hivyo ni vidogo na vitawachukua zaidi ya miaka 10 kila mmoja kuweza kulipa kiasi cha zaidi ya sh milioni 3.02 anazopaswa kulipa.
“Kimsingi madai haya yanatokana na kesi ya madai ambayo mtu anayeifungua anajua kuwa endapo anashindwa kuna gharama atapaswa kuzilipa, hivyo kutumia kipindi kirefu kulipa deni hilo mahakama haitaona kama yule aliyeshinda kesi amepata matunda ya ushindi wake, kulipa deni hilo kwa miaka 16 ni kipindi kirefu mno na kitapoteza muda wa mahakama katika kufuatilia,” alisema hakimu Magesa.
Hivyo akaagiza deni hilo lilipwe kwa mikupuo miwili huku akiutaka upande wa waleta maombi kwenda gerezani kuleta mchanganuo wa gharama za kumhudumia mfungwa ili kama wakishindwa kutekeleza amri hiyo ya mahakama waweze kupelekwa huko.
Wakili kimomogoro alielezea kuridhishwa na uamuzi huo ambapo alionyesha barua aliyopewa na mkuu wa gereza la mkoa wa Arusha ambapo ilionyesha kuwa mfungwa mmoja hutumia kiasi cha sh 11,400 kwa siku kwa ajili ya chai, chakula cha mchana na jioni, matunda na maji ya kunywa.
Kwa upande wao, madiwani hao waliotimuliwa CHADEMA walielezea kuridhishwa na uamuzi wa mahakama ingawa walionesha masikitiko yao dhidi uamuzi wa CHADEMA wa kuamua kuwadai fidia wakati hata wao walichangia katika kukijenga chama hicho.
Agosti 10 mwaka jana, mahakama ya hakimu mkazi mkoa iliyokaa chini ya hakimu Hawa Mguruta, ilitupilia mbali shauri la madai lililofunguliwa na madiwani hao dhidi ya Mbowe na CHADEMA baada ya kubaini kuwa kulikuwa na mapungufu ya kisheria.

No comments:

Post a Comment