USHINDI wa kishindo ambao ameupata Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira katika nafasi kumi za ujumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, unaelezwa kuwa unatokana na yeye
kutokuwa katika kambi yoyote iliyopo katika chama hicho.
Vilevile,
ushindi wa Wassira ambaye aliibuka kidedea kwa kuzoa kura
2,135,unatokana kumudu jukwaa wakati wa kujieleza na kuonyesha kuwa yeye
ni mwarobaini kwa wapinzani hususan Chadema.
Wakati akijinadi
mbele ya wajumbe kabla ya kupigiwa kura, Wassira aliomba apewe nafasi
hiyo ya ujumbe wa Nec, ili apeleke kilio Chadema.
“Nipeni kura
nipate nafasi ili nipeleke kilio Chadema,” alisema Wassira huku
akishangiliwa wakati akiomba kura na Rais Jakaya Kikwete akimwita kwa
jina la utani, Tyson.
Baadhi ya makada wa CCM waliliambia gazeti
hili kwamba kete ya kuwashughulikia Chadema, ‘ilimbeba’ Wassira
ikizingatiwa kwamba chama hicho cha upinzani ndicho kinachowakosesha CCM
usingizi.
Wassira ambaye aliwahi kuwa mbunge wa upinzani kupitia
Chama cha NCCR-Mageuzi, hivi sasa ni mmoja kati ya makada tegemeo wa
CCM na katika siku za karibuni amekuwa mstari wa mbele katika shughuli
zote za chama hicho hasa za utatuzi wa migogoro na pale chama chake
kinapohitaji utetezi mbele ya vyama vya upinzani.
Miongoni mwa
shughuli hizo ni kuwa mmoja wa walioongoza kampeni za CCM katika chaguzi
ndogo za Igunga na Arumeru Mashariki, ambako alitumia muda mrefu
kukishambulia Chadema na viongozi wake. Pia kushughulikia mgogoro ndani
ya CCM mkoani Arusha na bungeni amekuwa akiongoza kujibu hoja za
wapinzani, ingawa umma umekuwa ukikosoa kauli zake za mara kwa mara.
Habari
zilizopatikana zinaeleza kwamba sababu nyingine ya Wassira kupata kura
nyingi ni kutokana na yeye kutokuwa katika kambi ya makundi ya kuusaka
urais wa 2015 yaliyopo ndani ya CCM.
Pia nafasi yake ya uwaziri
anayehusika na mambo ya siasa, inatajwa kwamba imempa nafasi ya kuwa
karibu na viongozi wengi wa CCM kuanzia ngazi ya taifa hadi wilayani.
Mjumbe
wa Mkutano Mkuu, kutoka Mkoa wa Morogoro, Semindu Pawa alisema kuwa
ushindi wa kishindo wa Wassira unatokana na yeye wakati wa kiujieleza
kumudu jukwaa.
Semindu Pawa ambaye ni Mbunge wa zamani wa
Morogoro Kusini Mashariki alisema, Wassira alijua namna ya kutumia muda
kwani alikuja na kauli ambayo iliwafurahisha wajumbe ya kueleza kuwa
apewe nafasi hiyo ili apeleke kilio kwa Chadema.
No comments:
Post a Comment