Friday, November 16, 2012

Safu ya Mkapa yarejea CCM

KUNA kila dalili kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amekirejesha chama hicho katika mikono ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, baada ya kuwateua katika nafasi za juu za CCM waliokuwa wasaidizi wa mtangulizi wake huyo.
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye inadaiwa ameshinikiza kurudishwa kwa safu yake ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) lengo ikiwa ni kukinusuru chama na Serikali yake  Mwananchi
Wasaidizi hao ni pamoja na Makamu Wenyeviti, Philip Mangula (Tanzania Bara) na Dk Ali Mohamed Shein (Tanzania Zanzibar) pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, ambao walichaguliwa na kuteuliwa katika vikao vya juu vya CCM vilivyomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba lengo la mabadiliko yaliyofanywa ni kujaribu kurejesha utaratibu wa CCM kuisimamia Serikali, utamaduni ambao ni kama ulikuwa umekufa, tangu Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani.
Mhadhiri wa zamani wa Chuo cha Ushirika Moshi, Akwiline Kinabo anasema kwamba kuna kila dalili kuwa Mkapa ana ushawishi katika uteuzi wa safu mpya katika sekretarieti ya chama hicho.
“Inawezekana Mangula, Kinana na Dk Shein walifanya vizuri sana enzi za Mkapa hadi akashawishi waingizwe kwenye sekretarieti ya sasa, lakini enzi za Mkapa na sasa ni kama mlima na kichuguu,” alisema.
Kinabo ambaye katika uchaguzi wa CCM uliomalizika mwezi uliopita aligombea Nec kupitia Moshi Mjini na kushindwa, alisema viongozi hao hawawezi kwenda na kasi ya siasa za vijana wa sasa.
Kada huyo wa CCM alihoji, ”Hivi Kinana au Mangula wataweza kushindana na hoja za Halima Mdee na Zitto Kabwe majukwaani? Kuna vijana wengi wameshinda Nec kwa nini wasiingizwe huko?”
Naye mwasisi wa CCM na kada wa siku nyingi wa chama hicho, Steven Mashishanga alisema kuwa viongozi waliochaguliwa waliwahi kufanya vizuri siku zilizopita, hivyo hakuna shaka kwamba watarejesha utaratibu wa kutekeleza mwongozo wa chama wa 1981.
“Ukisoma mwongozo huo kuanzia ibara ya 81 utabaini kwamba kazi ya chama ni kuisimamia Serikali, hili lilikuwa halifanyiki kwa muda mrefu katika awamu ya nne, sasa hawa waliochaguliwa lazima waturejeshe katika msingi huo,” alisema Mashishanga ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mikoa ya Mwanza, Tabora na Morogoro.
Hata hivyo, alisema wasiwasi wake ni iwapo uongozi mpya utaweza kuleta mabadiliko kutokana na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho kujaa wabunge na mawaziri ambao hawawezi kuwa na ujasiri wa kuukosoa uongozi wa juu wa chama.
“Mimi kwangu msimamo unabaki kwamba chama ni chama na Serikali ni Serikali, huwezi kuwa chama na Serikali kwa wakati huohuo.
Sasa wewe jiulize, hivi waziri anaweza kukaa kwenye NEC akamkosoa mwenyekiti ambaye ni Rais wake? Hapo kuna kasoro ambayo tunapaswa kuirekebisha,” alisema Mashishanga.

No comments:

Post a Comment