Friday, May 24, 2013

Prof Jay: Sitaki hata udiwani!

Dar. Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule (Profesa Jay) amesema amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kukisaidia chama katika changamoto za kuikomboa nchi.
 
Akizungumza na Mwananchi jana Profesa J alisema hajajiunga na Chadema ili kugombea ubunge mwaka 2015, isipokuwa kwa dhumuni la kutaka kuongeza nguvu katika chama hicho akiwa kama kijana.
“Kujiunga na siasa si dhambi na haina maana kwamba nina mpango wa kugombea jimbo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Sihitaji kugombea hata udiwani ila ni kwa dhumuni la kutaka kuongeza nguvu katika chama ili kuyafikia malengo,” alisema.
Alisema yeye ni mfuasi wa Chadema tangu mwaka 2005 na amekuwa karibu na chama kwa nyakati nyingi lakini kwa sasa ameamua kuingia rasmi katika chama kama chachu katika kuongeza harakati kwa vijana.
“Nimeingia ili nisaidie hiki chama kuikomboa Tanzania kwani kwa muda mrefu niliokaa katika chama hiki nimegundua kuwa wamedhamiria kumkomboa msanii, kijana wa kawaida na wakubwa kwa wadogo hivyo nadhani nipo sahihi katika uamuzi wangu.”
“Natambua mimi ni mwanamuziki, sawa nina mashabiki wengi lakini haina maana kwamba sina haki ya kuchagua chama ninachoona mimi kinanifaa, lakini siwezi kusita kufanya kazi sehemu yoyote au wakati wowote chama kikinitaka nifanye kwa wakati husika,” alisema Profesa J.
Profesa J juzi alijiunga rasmi na chama hicho baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema mjini Dodoma na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi akiwa sambamba na msanii mwingine wa hiphop Kulwa Kinega maarufu kama K wa Mapacha ambaye alikabidhiwa kadi hiyo na Mbunge wa Ubungo John Mnyika.

JWTZ wakanusha taarifa za askari kujihusisha na makahaba DRC

  Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ, limekanusha taarifa zilizotapakaa kwenye mitandao kuwa askari wa jeshi hilo waliokwenda huko kwa ajili ya kulinda amani,wameanza kujihusisha na makahaba.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Mtandao wa www.congodrcnews.com wanajeshi wa Tanzania wameanza kujihusisha na ubakaji wanawake katika Mji wa Sake ulioko Goma.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa askari mmoja wa JWTZ alihitaji kujamiiana na mwanamke mmoja(Kahaba) kwa ujira wa Dola 50. Baada ya kumaliza shida zake ambazo ilielezwa alizifanya bila kinga yoyote,askari huyo alikataa kumlipa ujira wake,hali iliyoleta tafrani na mwanamke huyo kupiga kelele.
“JWTZ linapenda kuwaeleza wananchi kuwa taarifa hizo ni za uongo mtupu wenye nia ya kulipaka matope JWTZ na Tanzania kwa ujumla. “Picha iliyotolewa kwenye tovuti hiyo ya www.congodrcnews.com ni ya wanajeshi wa Tanzania walipokuwa katika Operesheni ya huko Comoro mwaka 2008.
Mtu anayeonekana kuwa chini ya Ulinzi alikuwa ni mshiriki wa Kanali Mohamed Bacar ambaye aliondolewa madarakani.
“Vilevile picha hiyo ilitolewa vile vile katika tovuti za www.apc.net.au/news/stories ya Machi 26, 2008 na ww.
Seattletimes.com. na pia picha hiyo ipo pia kwenye tovuti ya Jamii Forum baada ya kufanya ‘link’ kutoka kwenye Mtando wa www.google.com.”
Taarifa hiyo ilisema kuwa JWTZ inapenda kueleza wananchi na dunia kwa ujumla kwamba wanaoneza taarifa hizo wana lengo la kukatisha tamaa juhudi zinazofanywa na
nchi za Maziwa Makuu na SADC kuleta amani nchini DRC kwani JWTZ wako DRC kwa mujibu wa taratibu za kiutendaji za Umoja wa Mataifa.