Sunday, November 18, 2012

Mangula akunjua makucha asema atashughulikia rushwa CCM

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amekunjua makucha na kusema walioshinda katika chaguzi za chama hicho kwa rushwa wajiandae kung’olewa ndani ya miezi sita ijayo.
Mangula alisema hayo jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete katika sherehe zilizoandaliwa na mkoa wa Dar es Salaam kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwao.
“Wote walioleta malalamiko yanayohusu rushwa katika uchaguzi watulie, tunayashughulikia, kama kuna mtu alipita kwa rushwa afahamu kuwa amepoteza,” alisema Mangula ambaye anasema kabla ya kuteuliwa alikuwa anajishughulisha na kilimo cha nyanya na maparachichi.
Kauli hiyo nzito ya Mang’ula imekuja siku chache tangu kumalizika kwa chaguzi za ndani za CCM ambazo zililalamikiwa na baadhi ya makada kwamba baadhi ya walioshinda walitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua kura.
 
Miongoni mwa chaguzi zilizolalamikiwa ni katika baadhi ya wilaya na mikoa, lakini zaidi zile za jumuiya za chama hicho; Umoja wa Wanawake (UWT), Umoja wa Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi.
Itakumbukwa kuwa ni kutokana na hali hiyo, Rais alisema waziwazi wakati akifunga mikutano ya UWTna Wazazi na wakati wa kufungua ule wa UVCCM kwamba vitendo hivyo vitakipeleka chama hicho kubaya ikiwa havitakomeshwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema tayari chama hicho kimepokea malalamiko mengi kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi ndani ya chama hicho nyingi zikihusu rushwa lakini zaidi zinaztokana na chaguzi za jumuiya za chama hicho.
Mkakati wa Mangula
Jana Mangula alisema atatumia nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadili aliyopewa kuwang’oa waliopata uongozi kwa rushwa na kwamba “hatamwogopa kigogo yoyote wala hatamwonea mtu”.
Alisema watafanya uchunguzi wa kina kwa waliohusika na rushwa katika uchaguzi huo bila kuihusisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Hakuna mla rushwa atakayepona katika hili kwa sababu tunataka kurudisha heshima ya chama chetu ambayo imepotea kwa sababu ya walarushwa wachache,” alisema Mangula.
Aliongeza kuwa katika uchanguzi huo, hata waliokuwa wakisaidia kufanikisha rushwa hizo katika uchaguzi huo watachukuliwa hatua watakazostahili.
Mangula alisema anataka kuwaonyesha Watanzania kwamba hata wakulima wa nyanya wanaweza kufanya kazi ya kupambana na rushwa.
“Namshukuru Kikwete kwa imani yake aliyoionyesha kwangu hadi akaniteua kugombea nafasi hii,  sitamwangusha, nitamwonyesha kuwa hata wakulima wa nyanya wanaweza,” alisema Mangula huku akishangiliwa na halaiki ya wana CCM waliofurika kwenye viwanja hivyo.

No comments:

Post a Comment