Friday, November 23, 2012

Okwi, Ngassa, Twite watakiwa kwa Mil.300/

Emmanuel Okwi
Washambuliaji Emmanuel Okwi na Mrisho wa Simba pamoja na beki wa kimataifa Mbuyu Twite wa Yanga wanatakiwa kwa dau la jumla la Sh. Milioni 300 ili wazihame timu zao wakati dirisha la usajili wa dirisha dogo litakapofunguliwa rasmi, imefahamika.
Taarifa zilizothibitishwa jana, zimetaja mchanganuo wa ofa iliyotolewa kwa nyota hao kuwa ni dola za Marekani 50,000 kwa ajili ya kumtwaa Okwi, dola 40,000 za kumsajili Ngassa na beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite ametengewa dau la dola 100,000; hivyo jumla ya fedha zote kufikia dola 190,000 (Sh. Milioni 300).
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa klabu ya African Lyon inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Rahim Kangezi, alisema kuwa uongozi wa klabu yake ndiyo unaowataka wachezaji hao na tayari wameshaanza mawasiliano kwa kuziandikia barua klabu za Simba na Yanga kwa nia ya kujaribu kufanya nao biashara, lakini hadi sasa bado hawajajibiwa.
Kangezi alisema kuwa klabu yao ambayo iko katika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi, iko kutoa fedha hizo ili kuwatwaa nyota hao kwa vile wanajua kuwa watawasaidia kutimiza malengo yao.
"Tayari tumeshampa barua Kaburu (Geofrey- Makamu Mwenyekiti wa Simba) ila wanaonekana hawataki kutupa ushirikiano… kuna wadau tumewapata ambao ndiyo wanatoa fedha hizo," alisema Kangezi, ambaye ndiye alifanikisha usajili wa kiungo Nizar Khalfan kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada kabla hajahamia Philadephia Union na baadaye kurejea nchini kuichezea Yanga.
Kangezi aliongeza kwamba wadau wao ambao ndiyo wanaoisaidia Lyon wanataka kuona timu hiyo inaendelea kushiriki kwenye ligi ya Bara na ndiyo maana wameahidi kuisaidia fedha za kusajili wachezaji zaidi watakaowaongezea nguvu kikosini na kutimiza lengo la kuibakiza timu yao ligi kuu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, aliliambia gazeti hili kwamba hawako tayari kumuuza mchezaji wao yeyote ikiwa wanunuzi hawajafikia vigezo vyao, ikiwa ni pamoja na kutanguliza ofa ya maana ya walau dola za Marekani 200,000 (Sh. Milioni 315).
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga na katibu mkuu wake wake, Evodius Mtawala hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo huku Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akishindwa kulielezea baada ya kusema kuwa yeye na viongozi wengine wa klabu yake wako katika kikao cha kamati ya utendaji.
Katika hatua nyingine, Kangezi alisema kuwa licha ya kutokuwapo na muafaka kati yao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), bado wadhamini wao (Zantel) wanaendelea kuwapa fedha na wiki ijayo wachezaji wataanza mazoezi kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment