Friday, November 16, 2012

Membe: Niliponea chupuchupu

MJUMBE  wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Bernard Membe amekiri kuwa haikuwa rahisi kwake kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kupitia kundi la kifo kwa kuwa upepo uligeuka ghafla kinyume na matarajio yake.

Membe ni miongoni mwa makada wa CCM waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Nec kupitia nafasi kumi zilizokuwa zikiwaniwa na vigogo kadhaa wa chama hicho.

Akizungumza na Mwananchi jana, Membe alisema kuwa amefurahishwa na matokeo yote na kwamba ushindi wake wa kupata nafasi kati ya washindi kumi ni salamu kwa waliokuwa wakipiga kampeni chafu dhidi yake.

“Ninawashukuru wajumbe wote wa Mkutano Mkuu kwa kunichagua… Kuchaguliwa kwangu kumetuma ujumbe mzito kwa waliokuwa wakihaha kuhakikisha kwamba, sipati nafasi hiyo kwa gharama zozote,” alisema Membe.

Makada wengine waliochaguliwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Wengine ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Fenella Mukangara.

Membe alishika nafasi ya sita katika kundi hilo licha ya vitisho kutoka kwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CC, Hussein Bashe ambaye siku moja kabla ya uchaguzi aliapa kuwa  atahakikisha waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ‘hapiti’.

Baadhi ya watu walio karibu na Membe wanasema kuwa, mambo yalibadilika ghafla mjini Dodoma siku ya Jumamosi baada ya waziri huyo kuongozana na Rais Jakaya Kikwete kwenda mkoani Shinyanga kwenye mazishi ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Hayati Aloysius Balina.

“Baada ya Mheshimiwa Membe kuondoka kwenda Shinyanga, wapinzani wake ndani ya chama walitumia muda huo kupiga propaganda mbaya dhidi yake na walianza kutangaza hadharani kwamba, hatapata nafasi hiyo ili kumnyong’onyesha,”  kilisema chanzo chetu ambacho hakikutaka kutajwa gazetini.

Membe ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaotajwa kuanza kujijenga kwa ajili ya kuwania urais 2015 kupitia CCM na kundi lake limekuwa likisigana na la kada mwingine anayetajwa kuwania nafasi hiyo, Edward Lowassa.

Aidha, kumekuwa na minong’ono mingi baada ya yeye kushika nafasi ya sita katika kundi la watu kumi kwamba ameanguka kisiasa, lakini yeye anasema amefanikiwa.

Membe alisema kimsingi kila aliyeomba kuchaguliwa kupitia mkutano mkuu alikuwa na matumaini ya kushinda japokuwa wengine hawakufanikiwa.

“Unajua, inabidi yeyote anayetaka kunipima ajue kwamba, sikugombea ili nishike namba moja, la hasha; niligombea kuchaguliwa kuwa mjumbe wa NEC na ninamshukuru Mungu nimepata,” alisema Membe.

JK anena
Katika hatua nyingine Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, jana alitoboa siri kuwa, wapo watu waliokuwa wakitambika usiku na mchana ili chama hicho kitoke vipande kwenye Mkutano Mkuu wa nane.

Akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM mkoani Dodoma katika sherehe maalumu iliyoandaliwa na uongozi wa mkoa huo kuwapongeza viongozi wapya, Kikwete alisema mkutano huo umekwisha kwa mafanikio kinyume na matarajio ya wengi.

Alisema CCM sasa kiko imara na tayari kimekwishapanga safu yake kwa ajili ya mapambano na kwamba, uchaguzi huo ni ujumbe tosha kwa wapinzani.

“Nashukuru Mungu mkutano umeisha salama maana kulikuwa na watu walikuwa wakisali na hii si kusali bali ni kutambika usiku na mchana ili kwenye mkutano mkuu kuwe na vipandepande,  lakini haikuwa hivyo kabisa mkutano umeisha salama bila ya matatizo yoyote,” alisema.

Kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Mkutanmo Mkuu alisema, watayachambua maazimio na mapendekezo yote na kuyatengenezea mpango utekelezaji ndani ya chama na Serikali.

Aliwatwisha jukumu zito wajumbe wa NEC kuwa mara baada ya mafunzo watatakiwa kutembea nchi nzima kwa ajili ya kueneza sera za chama na kueleza ukweli juu ya CCM kwa  Watanzania.

“Ili kufikia malengo niliyoyataja, lazima tuanze na Wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ambao wao wakipata mafunzo watakuwa wakufunzi wa wengine,” alisema Kikwete.

Sekretarieti kazini
Katika hatua nyingine Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema Sekretarieti mpya iliyoteuliwa juzi imeanza kazi kutekeleza majukumu yake.

Alipoulizwa kama sekretarieti hiyo ina uwezo wa kuendelea kufanya kazi bila ya kuundwa kwa Kamati kuu, Nape alisema hilo siyo jambo la kushangaza.

“Nakwambia Sekretarieti mpya inaendelea na kazi zake na ilianza kazi mara tu baada ya kuteuliwa juzi,” alisema Nape.

Alipoulizwa ni kazi zipi zilizokwishafanywa na wajumbe wa kikao hicho, Nape alisema ni kazi za kawaida kama zilivyoainishwa katika katiba ya chama hicho.

“Tunaendelea na kazi za kawaida za chama, nenda kaangalie katika katiba utaona kazi za kila mjumbe zimeainishwa kule,” alisema na kukata simu.

No comments:

Post a Comment