Friday, November 23, 2012

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) vinatarajia kuvamia mikoa yote nchini kwa ajili ya kukutana na wananchi.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) vinatarajia kuvamia mikoa yote nchini kwa ajili ya kukutana na wananchi.
CCM kimetangazwa kwamba kitaanza ziara hiyo katika mikoa minne kuanzia kesho huku safu yake mpya ikiongozana na mawaziri.
Nacho Chadema kimetangaza kuwawapeleka viongozi wake wa juu katika mafunzo ya kuwajengea uwezo kabla ya kuanza operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari mwakani.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mawaziri wa Wizara mbalimbali kesho wanatarajia kuanza kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya mwaka mwaka 2010.
Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa, ziara hiyo iinatarajia kuanza katika mikoa ya Mtwara, Geita, Rukwa na Arusha.
Alifafanua kuwa katika ziara hiyo, Kinana atapata maelezo ya kina juu ya utekelezaji wa Ilani hiyo.
“Ni muhimu Mawaziri kuelezea juu ya utekelezaji wa Ilani kwa kuwa Chama hiki ndicho chenye mkataba na wapiga kura, hivyo lazima kiwabane mawaziri wa serikali inayotokana na Chama hiki ili kuitekeleza,” alisema Nape alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema ziara hiyo ni miongoni mwa maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliomalzika hivi karibuni mkoani Dodoma.
Hii ni mara ya pili CCM kufanya ziara mikoani ikiwa na Mawaziri. Mapema mwaka huu, viongozi hao walizunguka maeneo mbalimbali ya nchi kuelezea utekelezaji wa Ilani kwa wananchi.
Kwa upande wake, Chadema kimeanzisha mpango wa kuwapa mafunzo viongozi wa kitaifa na watendaji wa Makao Makuu pamoja na wenyeviti na makatibu wa mikoa ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya maandalizi ya operesheni ya M4C itakayoanza kutikisa nchi Februari 2013.
Katika orodha hiyo, wamo wenyeviti na makatibu wa mikoa wapatao 64 na baada ya mafunzo hayo, chama hicho kwa siku kitakuwa kinafanya mikutano ya hadhara 239 katika vitongoji, vijiji, kata na wilaya kwenye mikoa yote nchini ili kuimarisha mchakato wa mabadiliko.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa Chadema, Benson Kigaila, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema mafunzo hayo ambayo yataanza Novemba 22 hadi 23 mwaka huu, pia yatahusisha viongozi wa kitaifa na watendaji wa Makao Makuu.
Kigaila alisema siku mbili za mafunzo hayo ambayo yatafanyika Wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera, zitakuwa ni kwa ajili ya mafunzo ya darasani na baada ya hapo wenyeviti na makatubu hao watasambazwa katika vitongoji na vijiji vya wilaya hiyo kufanya mikutano ya hadhara.
“Mafunzo haya ya darasani na vitendo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya ujenzi na uimarishaji wa Chama, hususani kupitia Vuguvugu la Mabadiliko ambayo moja ya malengo yake ni kuwajengea uwezo viongozi kwa kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara,” alisema Kigaila.
Kigaila alisema baada ya mafunzo hayo, wenyeviti na makatibu hao watarudi katika maeneo yao kwenda kutoa mafunzo kwa wilaya na majimbo yote ya mikoa ambao nao pia watashusha elimu hiyo kwenye kata, vijiji na vitongoji.
Alisema baada ya mafunzo hayo kufikia katika ngazi ya chini ya uongozi wa chama, operesheni M4C itakuwa inafanyika kwa ngazi zote nchi nzima kwa kufanya mikutano ya hadhara 239.
“Tunataka kuwasha moto nchi nzima ili tuone kama CCM watakuwa na ubavu wa kujibu mapigo kama ambavyo wameelezwa kuwa wawe wanajibu mapigo ya wapinzani,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment